KIKOSI cha 'Walima Zabibu' kinachomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dodoma Jiji FC kimepiga kambi Mkoani Morogoro "Mji kasoro Bahari" ili kujiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2021/2022.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye uwanja wa Chuo cha Ualimu Morogoro ambapo ndipo timu hiyo inapofanyia mazoezi Afisa Habari wa Klabu hiyo Moses Mpunga amesema kuwa kambi hiyo itakua ni ya siku 14 na kwamba wameamua kuweka kambi hapo kutokana na hali nzuri ya hewa na utulivu wa hali ya juu ambao utawasaidia wachezaji kutulia na kufanya maandalizi vizuri kuelekea kwenye msimu mpya wa Ligi hiyo.
Mpunga ameongeza kuwa tayari asilimia 95 ya wachezaji wapo kambini huku akiwataja baadhi ya wachezaji wapya waliosajiliwa na timu hiyo katika dirisha kubwa la usajili msimu huu kuwa ni sehemu ya kikosi hicho Mkoani humo.
“Tayari kikosi chetu kipo Morogoro, wachezaji wetu wazamani na baadhi wapya wameshaanza mazoezi chini ya Kocha Mkuu Mbwana Makata wachezaji wapya ambao wapo kambini tayari ni Emmanuel Martin, David Ulomi na golikipa Mohamed Yusuph” alisema Mpunga.
Aidha akizungumzia hali ya kikosi kwa ujumla Mpunga amesema kuwa wachezaji wanaendelea vizuri na hakuna majeruhi yeyote katika kambi yao.
Mpaka sasa Dodoma Jiji FC imeshazinyaka saini za wachezaji sita ambao ni washambuliaji Emmanuel Martin na David Ulomi, kiungo Hussein Nassoro, beki Joram Mgeveke, na magolikipa Mohammed Yusuph pamoja na Rahim Sheikh.
Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2021/2022, inatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu wa tisa huku timu mbalimbali zikijichimbia katika Miji tofauti nchini na zingine nje ya nchi ili kujiandaa na Ligi hiyo.
Baadhi ya picha za wachezaji wa timu ya Dodoma Jiji FC wakiwa mazoezini kwenye kambi waliyoweka mjini Morogoro
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.