KIKOSI cha Dodoma Jiji FC chenye wachezaji, benchi la ufundi na viongozi leo kimeanza safari ya kuzifuata alama tatu Jijini Dar es salaam ambapo watakutana na Simba SC katika mchezo wa ligi kuu namba 245 kwenye dimba la Mkapa Jijini humo majira ya saa 1:00 usiku.
Dodoma Jiji ambayo imepanda daraja msimu huu imekuwa na wakati mzuri katika mzunguko wa pili wa ligi Kuu Tanzania Bara kwa kucheza michezo tisa na kuwa na wastani mzuri wa matokeo kitu ambacho imekua chachu kwa wapenzi soka Jijini Dodoma na wachambuzi wa masuala ya soka wanaitabiria makubwa timu hiyo ya makao Makuu ya Nchi.
Akizungumzia safari hiyo Afisa Habari wa timu hiyo Moses Mpunga amesema kuwa kikosi kipo katika hali nzuri na mwalimu amewaandaa wachezaji kulingana na umuhimu wa mchezo huo kwani wanahitaji alama tatu ili wazidi kujihakikishia nafasi ya kubakia katika ligi Kuu, hivyo mchezo huo ni muhimu sana kwao.
“Simba ni timu kongwe tunaiheshimu ila kwenye soka ukongwe sio sababu ya kutuzuia kupata alama tatu kwao, tunaamini kwa ubora wa mwalimu na wachezaji wetu tunaweza kuondoka na alama tatu, najua asilimia kubwa wanaipa Simba kipaumbele lakini tutawashangaza” amesema Mpunga.
Akizungumzia kuhusu wachezaji watakaoukosa mchezo huo Mpunga amemtaja Salmin Hoza ambae bado anaumwa na anaendelea na matibabu pamoja na Rajab Mgalula ambae amekua akisumbuliwa na goti kwa muda mrefu ila waliobaki wote wako vizuri na mwalimu ataangalia ni nani atahitaji kumtumia kwenye mchezo huo.
Dodoma Jiji wanakutana na Simba kwa mara ya pili katika msimu huu wa 2020/2021 ambapo katika mchezo wao wa kwanza walipoteza kwa 2 – 1 wakiwa nyumbani.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.