WAKALI wa Makao Makuu ya Nchi, 'Walima Zabibu' Dodoma Jiji FC wameshindwa kuutumia vyema uwanja wao wa nyumbani kwa kukubali kufungwa na Simba SC ikiwa ni mchezo wa pili tu wa msimu mpya wa ligi Kuu Tanzania Bara 2021/2022 katika mchezo ulioonekana kuwa wa kasi na wenye matumizi makubwa ya nguvu na ubabe kwa timu zote mbili. Kikosi cha Dodoma Jiji kilionekana kuwa bora sana katika kipindi chote cha kwanza ila mambo yakabadilika baada ya mshambuliaji wao Anuary Jabir kupewa kadi nyekundu hali iliyowalazimu 'walima zabibu' hao kucheza pungufu na kupelekea Simba kupata goli katika kipindi cha pili kupitia kwa Meddie Kagere.
Akizungumza na wanahabari mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Mbwana Makata amewapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kuonesha ushindani mkubwa licha ya uchache wao uwanjani. Makata ameongeza kuwa walikua na nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo lakini mambo yalibadilika baada ya kadi nyekundu ambayo ilimlazimu kubadili mfumo wa kiuchezaji kutokana na uchache wao ili kuweza kuendana na mchezo. "Unapokutana na hizi timu kongwe kuna mambo mengi hutokea ambayo yanaweza kukulazimisha kubadili mfumo wako wa kiuchezaji ila licha ya hayo yote bado tulionekana kuwa imara mpaka mwisho wa mchezo" alisema Makata.
Kwa upande wake Afisa Habari wa Dodoma Jiji Moses Mpunga amewashukuru mashabiki wao kwa kujaa uwanjani jambo ambalo liliongeza hamasa kwa wachezaji na kuwadhoofsha wapinzani wao kwani kwa mara ya kwanza mashabiki wa timu hiyo waliingia kwa wingi uwanjani na kushangilia tofauti na ilivyozoeleka kuwa Simba na Yanga zinapokuja huwa ni ngumu kuuona wingi wa mashabiki wa Dodoma Jiji. "Tumeweka historia katika soka la Nchi hii ni ngumu sana kuwaona mashabiki wa timu nyingine kwa wingi pale wanapocheza na Yanga au Simba ila sisi kwa mara ya kwanza tumewanyamazisha tulijaa uwanjani, hamasa iilikua kubwa ikiongozwa na Mhe. Mbunge wetu Anthony Mavunde, na hili sio kwa mechi hii tu ila ni kwa mechi zote za nyumbani" aliongeza Mpunga. Hata hivyo Mpunga amesema kuwa mchezo huo umekwishamalizika na sasa wanautupia macho mchezo wao wa tatu dhidi ya Mbeya Kwanza ambao watakua ugenini Jijini Mbeya tarehe 17/10/2021.
Kwa sasa Dodoma Jiji inashika nafasi ya nane katika msimamo wa ligi ikiwa na alama tatu huku ikicheza michezo miwili, ikishinda mmoja na kupoteza mmoja.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.