WALIMU wa Shule za Msingi na Sekondari zilizopo kata ya Ipagala Jijini Dodoma wamepongezwa kwa ufaulu wa wanafunzi wao katika mitihani ya Taifa kwa mwaka 2021/22.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mh. Omar Juma Kipanga wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo kwa walimu na wanafunzi wa kata Ipagala kufuatia hafla fupi iliyoandaliwa na Diwani wa Kata ya Ipagala Mh. Gombo Kamuli Dotto kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mh. Anthony Mtaka na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Mh. Anthony Mavunde.
“Niwapongeze sana walimu kwa kazi nzuri mnayoifanya, haya ni matokeo mazuri ya ushirikiano mzuri kati ya walimu, viongozi na wazazi.
Tunamshukuru Mh. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma ambacho pia kinawagusa na ninyi walimu ikiwa ni sehemu ya kuthamini mchango wenu mkubwa katika maendeleo ya elimu.” Alisema Kipanga.
Akitoa maelezo ya awali Diwani wa Kata ya Ipagala, Mh. Gombo Kamuli Dotto amesema imekuwa ni utaratibu kwa kata hiyo kuwapongeza na kutoa tuzo kwa walimu na wanafunzi pindi wanapofanya vizuri na kuongeza morali ya kufanya vizuri zaidi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mh. Anthony Mtaka ameitaka jamii kuthamini kazi nzuri inayofanywa na walimu na kuunga mkono jitihada za mkoa wa Dodoma katika kuinua viwango vya elimu kwa kuifanya Dodoma kinara wa elimu siku chache zijazo.
Mbunge wa Dodoma Mjini, Mh. Anthony Mavunde na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini kwa pamoja wamepongeza hatua hii ya kuenzi mchango mkubwa wa walimu na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha katika kuendeleza sekta ya elimu Jijini Dodoma.
Pamoja na vyeti vya shukrani walivyopewa, walimu hao pia watapata fursa ya kutembelea Ngorongoro crater ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kukuza sekta ya Utalii nchini.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mh. Omar Juma Kipanga wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo kwa walimu na wanafunzi wa kata Ipagala Jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.