Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WALIMU wakuu wa shule za msingi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kuwa wanahudhuria vikao vya kamati za maendeleo za kata ili kuwasilisha changamoto zinazozikabili shule zao na kupatiwa ufumbuzi.
Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira, Jaffar Mwanyemba alipoongoza Kamati ya Fedha na Utawala ‘route one’ kutembelea na kukagua ujenzi wa madarasa mawili ya shule ya msingi Mbwanga iliyopo katika Kata ya Mnadani jijini hapa.
Mwanyemba alishauri kuwa walimu wakuu wawe wanahudhuria kamati za maendeleo za kata. Kamati za maendeleo za kata ndiyo sehemu ambayo changamoto za shule za msingi zinaweza kujadiliwa kwa karibu na kuwekwa katika vipaumbele vya kata.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mbwanga, Mwalimu Aloyce Muyinga alisema kuwa shule yake ilipokea shilingi 40,000,000 Novemba, 2021 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa. “Hadi sasa shilingi 36,600,000 zimetumika kwenye ujenzi. Shilingi 3,400,000 zipo katika akaunti. Mradi umefikia hatua ya umaliziaji na vifaa vilivyokosekana ni vioo. Mradi unakabiliwa na changamoto ya mfumuko wa bei, jamii na kamati kuhitaji fedha kama zawadi” alisema Mwalimu Muyinga.
Alisema kuwa shule yake ina vyumba vya madarasa 11, wakati mahitaji ni madarasa 57 na upungufu madarasa 46. “Shule ina matundu ya vyoo 16 tu, wavulana matundu 8 na wasichana matundu 8, upungufu wavulana matundu 41 na wasichana upungufu matundu 57 jumla ya mahitaji ni 114” alisema Mwalimu Muyinga.
Ikumbukwe kuwa shule ya msingi Mbwanga ina jumla ya wanafunzi 2,607 kati yao wavulana ni 1,294 na wasichana ni 1,313 iliwa na walimu 42, wanaume wanne na wanawake 38.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.