Sifa Stanley na Constantine Binde, DODOMA
WALIMU wanaofundisha somo la kiingereza katika shule za sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kujipanga kujenga umahiri wa somo hilo kwa wanafunzi ili wabobee katika lugha hiyo.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alipokuwa akifungua semina kwa walimu wanaofundisha somo la kiingereza wa shule za sekondari jijini hapa na kufanyika katika shule ya sekondari Dodoma.
Mwalimu Rweyemamu aliwataka walimu kuchukua hatua ambayo itasaidia kujenga umahiri wa somo la kiingereza kwa wanafunzi. Aliitaja hatua hiyo kuwa ni kuanzisha sera ya kuzungumza kiingereza (English Speaking Policy) muda wote wanafunzi wanapokuwa shuleni. “Tuwasiliane kwa kutumia lugha hii. Mimi naamini sana katika kujaribu. Mara kwa mara tuwakazanie kuongea kiingereza, tuanzishe hata sera ya kuzungumza kiingereza muda wote wa masomo. Tuwasaidie wanafunzi wazungumze lugha hii” alisema Mwalimu Rweyemamu.
Mkuu huyo wa idara alisema kuwa semina hiyo itasaidia kuwaweka pamoja walimu wa somo la kiingereza na kujadili mbinu mbalimbali za kufundisha somo hilo. “Semina hii itaunganisha walimu kutoka shule mbalimbali na wataalamu kutoka TELTA ambao watasaidia kufundisha mbinu hizo kwa walimu wengi” alisema Mwalimu Rweyemamu.
Naye muwezeshaji wa semina hiyo, Mwalimu Anne Nyambi alisema kuwa semina itaunganisha walimu wa somo la kiingereza Tanzania ili wajue mambo muhimu yahusuyo lugha ya kiingereza. “Kama tunavyojua, lugha hii ni ngeni hivyo, ni muhimu sana kuwa pamoja na kushirikishana mambo mbalimbali ili wanafunzi wetu tunapowafundisha tuwafundishe vitu ambavyo ni sahihi na vyenye kufanana” alieleza Mwalimu Nyambi.
Semina ya kuwajengea umahiri walimu wa kiingereza wa shule za sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliandaliwa na chama cha walimu wa somo la kiingereza Tanzania (TELTA).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.