RISALA iliyosomwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Mkoa wa Dodoma wakati wa maadhimisho ya Sherehe za Mei Mosi Mwaka huu imeeleza jinsi wafanyakazi wa Wizara na Taasisi mbalimbali zilizohamia Makao Makuu ya Nchi Dodoma kutoka Dar es Salaam walivyofurahishwa na upatikanaji wa viwanja vya Makazi vilivyopimwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Risala hiyo ilisomwa wakati wa sherehe hizo zilizofanyika uwanja wa Jamhuri Jijini hapa mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge, ambapo viongozi mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa Wabunge na Mawaziri pia walihudhuria.
Aidha, pamoja na kuelezea furaha yao, wafanyakazi kupitia Shirikisho lao wameomba kuongezewa muda wa kulipia viwanja walivyonunua kufikia miaka mitatu badala ya miezi mitatu kutokana na hali ya kiuchumi kwa Wafanyakazi wengi kuwa ya kawaida.
Akizungumza na umati wa Wafanyakazi wa Serikali, Sekta Binafsi na wakazi wa Jiji la Dodoma waliofurika katika uwanja Jamhuri, Dkt. Mahenge aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kupima viwanja vya matumizi mbalimbali kwa kasi inayoendana na mahitaji ya Dodoma ya sasa ambayo ni Makao Makuu ya Nchi.
Akijibu ombi hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Mahenge aliahidi kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi kuweka utaratibu kwa makundi mbalimbali na watu binafsi kupewa muda wa kutosha wa kulipia kiwanja kulingana hali ya kiuchumi ya Wafanyakazi hao.
“Hata hivyo kuna baadhi ya maeneo ambayo ni lazima yaendelezwe haraka iwezekanavyo kutokana na mahitaji ya ukuaji wa Jiji kwa sasa, hivyo hili suala hatuwezi kulifanya kuwa la jumla” alifafanua Dkt. Mahenge.
Maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani kwa Mwaka huu yaliongozwa na kauli mbiu isemayo “Tanzania ya uchumi wa kati inawezekana, wakati wa mishahara na maslahi bora kwa wafanyakazi ni sasa”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.