MKUU wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama Mkoani Dodoma kuhakikisha vinawasaka na kuwabaini wote waliohusika na uchomaji moto katika bonde la mzakwe hii leo.
Senyamule alitoa agizo hilo mara baada ya kufika katika eneo hilo kujionea athari za uharibifu zilizosababishwa na moto ulioanza majira ya saa saba mchana.
Alisema asilimia 70 ya maji katika Jiji la Dodoma yanatoka katika bonde la Mzakwe na ni eneo la hifadhi hivyo ni muhumimu kukakikisha linalindwa na kuhifadhiwa kwa ustawi wa afya na mazingira ya watu wote.
Aidha, aliwapongeza vijana wa JKT Makutupora walioshiriki katika zoezi la kuzima moto uliotokea hii leo tarehe katika Bonde la Mzakwe Jijini Dodoma. Senyamule amewapongeza kwa uzalendo walionyesha wa kudhibiti moto huo na kuzuia usilete madhara makubwa, amesema wameonyesha uzalendo mkubwa, uhodari na ushupavu.
"Tumesikitishwa sana na moto huu kwa kuwa si kwamba umeathiri ikolojia ya eneo hili lakini pia umeharibu miundombinu ya Tanesco ikiwa ni pamoja na nguzo, hivyo kwanza nawapongeza vijana wetu kwa jitihada za kufanikisha kuzima moto huu na pili vyombo vyote vinavyohusika na uchunguzi vifanye kazi yake ili kubaini chanzo” Senyamule alisisitiza.
Aidha, Senyamule alimuagiza Meneja wa Bonde la Wami Ruvu kuhakikisha kuwa wanachonga barabara maalum kwa lengo la kukinga moto katika bonde hilo ili athari za moto zisiwe kubwa pindi moto utokeapo.
Awali Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Dodoma Julishaeli Mfinanga alisema kuwa walipata taarifa kwa njia ya simu kupitia namba za dharura 114 na kuwahi eneo la tukio kwa haraka. Amesema moto umedhibitiwa na hakuna madhara makubwa na wanaendelea na doria kuhakikisha usalama katika eneo hilo
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.