SERIKALI imeamua kutoa chanjo ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) kwa wananchi wake ili kuwaepusha na madhara yatokanayo na ugonjwa wa Korona na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa jana Oktoba 01, 2021 na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alipokuwa akiongea na wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi Dodoma (VETA) katika siku ya kwanza ya utekelezaji wa Kampeni ya kitaifa ya chanjo ya UVIKO-19.
Dkt. Method alisema kuwa Serikali imeamua kutoa chanjo ya UVIKO-19 kwa watu wote ili kuwalinda. “Hapa wengi wenu ni vijana, chanjo hii ni muhimu sana kwenu. Mkichanja mnajihakikishia usalama, lakini pia mnawahakikishia usalama na kuwalinda wazazi wenu huko nyumbani. Hivyo, suala la chanjo ni muhimu sana kwenu na kwa jamii mzima. Chanjo hii itawasaidia Watanzania kuokoa maisha yao na kuendelea kutekeleza majikumu yao ya kujiletea maendeleo” alisema Dkt. Method.
Mganga Mkuu huyo alisema kuwa ugonjwa wa UVIKO-19 unasababisha vifo kwa haraka sana. “Ndugu zangu, mtakubaliana nami kuwa madhara yanayosababishwa na ugonjwa wa UVIKO-19 ni makubwa. Madhara haya ni vifo na athari za kiuchumi” alisema Dkt. Method.
Kwa upande wa Mwalimu Filbert Ngilisho alisema kuwa ugonjwa wa UVIKO-19 ni hatari. Alishauri huduma ya kupata chanjo ni muhimu sana. “Serikali imetupa fursa ya kupata chanjo ya UVIKO-19, hivyo tutumie fursa hii vizuri” alisema Mwalimu Ngilisho.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeanza kutekeleza kampeni ya kitaifa ya chanjo ya UVIKO-19 kwa kutembelea taasisi mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha na kutoa huduma ya chanjo kwa watakaohamasika na kukubali kuchanjwa kwa hiari.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.