JIJI la Dodoma leo limegubikwa na vilio, majonzi, huzuni na machozi kila kona baada ya mwili wa aliyekua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyefariki Machi 17 mwaka huu kuwasili jijini Dodoma.
Mwili wa Hayati Dkt. Magufuli umewasili katika uwanja wa Ndege wa Dodoma majira ya saa 12:54 za jioni na kupokelewa na Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge, pamoja na viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama. Wananchi wa Jiji la Dodoma ambao licha ya mwili wa Hayati Dkt. Magufuli kuchelewa kufika, lakini bado walizidi kujipanga barabarani na kumsubiri shujaa wao bila kuchoka wakiimba nyimbo za maombolezo.
Wananchi wengi waliojumuika kwenye barabara za Jiji la Dodoma wakiimba "Jeshi, Jeshi, Jeshi," "Rais, Rais, Rais," "Baba, Baba, Baba," "Magu, Magu, Magu," huku wengine wakilia ni uthibitisho tosha kwamba Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alikua kipenzi cha watanzania na wana-Dodoma ambao amewafanyia mambo mengi ya maendeleo ikiwemo kuhamishia rasmi Makao Makuu ya Serikali Dodoma, kuipandisha iliyokuwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi, Soko Kuu la Job Ndugai, barabara za mzunguko, bustani ya mapumziko Chinangali, kituo cha kuegesha malori Nala, ujenzi wa barabara za lami kwenye mitaa mbalimbali na kadharika.
Wananchi wa Dodoma wameusindikiza mwili wa Hayati Dkt. Magufuli kutokea Uwanja wa Ndege kupitia maeneo ya Chako ni Chako, barabara ya Nyerere hadi mzunguko wa Jamatin, kisha kuelekea barabara ya Bunge, barabara ya Morogoro maeneo ya Chadulu, Ipagala, Nzuguni, Ihumwa, Mtumba hadi Ikulu ya Chamwino ambapo mwili wake utapumzishwa kwa usiku wa leo hadi kesho ambapo Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ataagwa rasmi kitaifa.
Kesho wananchi wa Jiji la Dodoma watapata fursa ya kushiriki shughuli ya kumuaga Hayati Dkt. Magufuli ambapo tukio hilo litafanyika kitaifa katika uwanja wa Jamhuri na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi likitanguliwa na zoezi la kumuombea na kuagwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.