WANAFUNZI takribani 130,000 wa shule za msingi ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma wenye umri kuanzia miaka mitano hadi 14 kupewa kingatiba kwaajili ya kuzuia ugonjwa wa Kichocho na kutibu Minyoo.
Hayo aliyasema Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alipokutana na wataalamu wa afya kwenye ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwaajili ya semina ya utoaji kingatiba kwa wanafunzi wa shule za msingi.
Dkt. Method alisema kuwa zoezi hilo ni la muhimu sana kwasababu linakwenda kuzuia magonjwa ambayo yamekua yakiathiri watoto kwa wingi kutokana na mazingira wanayoishi wengi wao wanapata matatizo ya minyoo ambayo yanapelekea kupata tatizo la upungufu wa damu.
“Tukiangalia katika kundi hili unakuta anatembea bila kuvaa viatu au amekula kitu hajanawa mikono hali inayopelekea kupata minyoo, tunaenda kutoa kingatiba ili kuhakikisha tunawalinda dhidi ya maambukizi maana wanapopata maambukizi wanashindwa kuhudhuria masomo yao hivyo, kupelekea kushuka kwa viwango vya elimu. Kwakupewa kingatiba tunawahakikishia ulinzi ili wasije kukosa shuleni kwa sababu ya kupata ugonjwa wa Minyoo au kupata ugonjwa wa Kichocho,” alisema Dkt. Method.
Dkt. Method alisema Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaenda kutoa kingatiba za aina mbili ambazo ni Albendazo kwaajili ya Minyoo na Praziquantel kwaajili ya ugonjwa wa Kichocho. Dawa za Kichocho zitatolewa kwenye kata nane ambazo ni Chigongwe, Chihanga, Ipala, Makutopora, Mbalawala, Mpunguzi, Nala na Mnadani. Alisema kuwa kata hizo zimeripotiwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa Kichocho.
“Kimsingi tunaenda katika kipindi cha mvua kunasehemu ambazo zina madimbwi ambayo ni maeneo rahisi kwa watoto kupata Kichocho, tunaenda kuwapa wanafunzi Kingatiba ili kuwalinda dhidi ya Kichocho. Nawashauri wazazi washirikiane na walimu kuhakikisha wanafunzi wanakula chakula katika kata zote zitakazopewa dawa ya Kichocho ili kuepusha wanafunzi wasije kuanguka kwasababu ya njaa,’’ alisema Dkt. Method.
Akiongelea namna walivyojipanga Mganga Mkuu huyo alisema kuwa Jiji la Dodoma limejipanga kuhakikisha wanafunzi wote wanafikiwa na kupewa kingatiba. Zoezi litafanyika kwa siku moja tarehe 24 na kutakuwa na siku ya ziada ya tarehe 25 kwaajili ya wanafunzi ambao walikosa shule kwa sababu mbalimbali, aliongeza.
“Tunawataalamu wa afya ambao wamepewa mafunzo pia tumetoa mafunzo kwa walimu katika shule za msingi ambao watashirikiana na wataalamu wa afya kuhakikisha kingatiba zinafika shuleni na wanafunzi wanapewa kwa usahihi. Wanafunzi watapewa kingatiba chini ya uangalizi wa walimu na wataalamu wa afya ili kuhakikisha wamekunywa kingatiba na wameweza kujilinda,’’ alielezea Dkt. Method.
Aidha, alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanafunzi wote wa shule za msingi wanafika shuleni siku ya tarehe 24 Novemba ili waweze kupata kingatiba akiwahakikishia kuwa hazina madhara yoyote ni salama kwa watoto.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.