Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MWENYEKITI wa timu ya Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Daud Mkhandi amewataka wanafunzi wa shule za sekondari kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu na kuchaguliwa katika shule za kitaifa.
Agizo hilo alilitoa alipoongoza timu ya Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mabweni na madarasa katika shule ya sekondari ya wasichana Bunge iliyopo jijini hapa.
Mkhandi alisema “tuwahamasishe wanafunzi kusoma sana na kufaulu ili waweze kuchanguliwa katika shule za sekondari za juu za kitaifa na kuweza kutoa mchango wao katika maendeleo ya taifa”.
Kwa upande wa Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prisca Myalla alisema kuwa jamii inatakiwa kuwasisitiza wanafunzi kusoma na kufaulu vizuri. “Mheshimiwa mwenyekiti, sisi halmashauri tutaendelea kusisitiza ufaulu mzuri kwa wanafunzi hasa kwenye shule za kata ili waweze kupangiwa shule za kitaifa kama hapa shule ya sekondari ya wasichana Bunge. Hakuna kigezo kingine zaidi ya viwango vya juu vya ufaulu” alisisitiza Myalla.
Awali Diwani wa Kata ya Kikombo, Emmanuel Manyono alisema kuwa shule ya sekondari ya wasichana Bunge kwa kuwa ipo Kata ya Kikombo, walitamani kuona watoto wa Kikombo wakipata fursa ya kusoma katika shule hiyo. “Tunatamani watoto wa Kikombo nao wanaofanya vizuri wawe wanachukuliwa hapa ili wananchi wetu wajivunie na kudumisha uhusiano mzuri na shule hii” alisema Manyono.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa mawili, mabweni mawili na viti na meza 60 kwa fedha za kuboresha shule za sekondari (SEQUIP), Mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana Bunge, Salome Mkombola alisema kuwa shule yake ilipokea shilingi 244,200,000. “Mgawanyo wake ulikuwa shilingi 200,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili, shilingi 40,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na shilingi 4,200,000 kwa ajili ya viti na meza 60” alisema Mkombola.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.