Na. Sekela Mwasubila, KONDOA MJI
WANAFUNZI wa kidato cha kwanza Katika Shule ya Sekondari Ula Halmashauri ya Mji Kondoa wametakiwa kuwa na nidhamu na kuzingatia sheria za shule walizopewa ili kuwa wanafunzi bora na kufanya vizuri katika masomo yao.
Hayo yamesemwa na Afisa Elimu Sekondari, Mwalimu Annette Nara alipokuwa akiongea na wanafunzi wa kidato cha kwanza waliopo katika shule hiyo wakati wa ziara ya ufuatiliaji aliyoifanya shuleni hapo.
“Kufaulu wote inawezekana ila ni jitihada zako mwenyewe kikubwa unapaswa kutunza nidhamu yako na kuepuka kujiingiza kwenye makundi ya utoro, ulaji wa mirungi na uvutaji wa bangi hawatakusaidia zaidi utapotea na ndoto zako,”amesema Mwalimu Nara.
Aidha, ameongeza kwa kuwaeleza kuwa wakumbuke wakifanya makosa ya utovu wa nidhamu mitaani watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za shule ambazo wanatakiwa kuzishika vizuri ili wapate matokeo mazuri na hawakufaulu kwa bahati mbaya.
“Mungu kakujalia ukafaulu hivyo soma kwa bidii kwa kuwa mwakani wana mtihani mna mtihani mwingine wa taifa wa kidato cha pili na maswali yote ya kiingereza ndio maana tunasisitiza pia kiingereza kitumike shuleni,”amesisitiza Mwalimu Nara
Aidha, amewasisitiza kutengeneza tabia ya kuongea kiingereza muda wote wanapokuwa shuleni si wanapomuona mwalimu tu kwani kwa kufanya hivyo hawataweza kujifunza na kuwataka kutoogopa kuchekwa kwa kuwa wanajifunza .
Amewaambia wanafunzi hao kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta fedha kwa ajili ya kuwa tengenezea mradi wa maji, kujenga madarasa mazuri na walimu wa kutosha hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kupata daraja la kwanza na la pili.
“Na nyie watoto wa kike ni marufuku kuvua sketi zenu kwa vijana huko mitaani na tukikujua umevua utalala gerezani kwa kuwa unakuwa umetutia aibu wanawake wote mlindane wenyewe kwa wenyewe mkiona mwenzenu anakuwa na tabia mbaya toeni taarifa kwa Mkuu wa Shule na nyie wanaume mtusaidie kuwalinda dada zenu kwa kuwa hapa kazi ni moja tu ya kusoma,”amesema Mwalimu Nara.
Mwisho Mwalimu amewapongeza walimu wa shule hiyo kwa bidii wanayoionyesha ambapo kwa matokeo ya mwaka huu wamepunguza idadi ya wanafunzi waliopata sifuri katika matokeo ya kidato cha nne ambapo mwaka 2021 wanafunzi 27 walipata sifuri na mwaka 2022 wanafunzi 14 pekee wamepata daraja 0 na kuwataka kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayepata sifuri kwa mwaka 2023.
Shule ya Sekondari Ula ipo katika kata ya Kondoa Mjini kwa mwaka 2023 imepangiwa wanafunzi 309 na hadi kufikia Februari mosi wanafunzi 234 wameripoti na wanafunzi 25 wamehama na jitihada za kuwatafuta waliobakia zinaendelea.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.