Na. Theresia Nkwanga, TAMBUKARELI
WANAFUNZI Shule ya Msingi Tambukareli watakiwa kuacha usiri na kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali katika kutokomeza matendo ya ukatili wa kinjisia.
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa Viti Maalum wa Jiji la Dodoma, Joyce George alipokuwa akiongea na wananchi wa Kata ya Tambukareli pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Tambukareli iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
George alisema kuwa serikali inafanya jitihada mbalimbali za kutokomeza ukatili wa kijinsia. Hivyo, wanafunzi hawapaswi kuogopa vitisho vya watu waliowafanyia ukatili wa kijinsia sababu serikali ipo nyuma yao kuhakikisha wanaoripoti taarifa za ukatili wa kijinsia wanalindwa.
“Kama unaogopa ukimripoti aliyekufanyia vitendo vya ukatili atakutukana na kukupiga niwaombe watoto wangu wazuri msiogope, msikubali kuzibwa midomo yenu kwa vitisho vyao huku mkiendelea kuvumilia maumivu makali ya ukatili wa kijinsia. Serikali ipo kwa ajili yenu imeweka vyombo vya sheria kuwasaidia katoeni ripoti kwa walimu wenu, wazazi, Polisi na kwa mtu yeyote wa karibu mnayemuamini. Msikubali kutishwa wala kuogopeshwa na mtu yeyote” alisema George.
Akielezea sababu za ukatili wa kijinsia kuendelea katika jamii, alisema kuwa Ukatili wa kijinsia kwa sehemu kubwa unafanywa na watu walio karibu. Hivyo, ili kumlinda ndugu huyo wa karibu, wahanga hawatoi taarifa ya vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa na kusababisha vitendo hivi vya ukatili kuendelea katika jamii zetu.
“Niwaombe ndugu zangu tuache kuwakumbatia wahalifu wa ukatili wa kijinsia hata kama ni ndugu zetu, hili janga haliwezi kuisha kama tutachagua kufumba macho na kukaa kimya. Toeni taarifa kwa vyombo vya dola, Serikali na hata asasi za kiraia pindi unapofanyiwa au kushuhudia vitendo vya Ukatili wa Kijinsia kwa msaada zaidi wa kisheria. Tukishirikiana kwa pamoja na kuvunja ukimya tunaweza kulitokomeza janga hili la ukatili wa kijinsia na kulikomboa Taifa letu” alisema George
Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalum Jiji la Dodoma, Leticia Sanga Aliwashauri wanafunzi wa Shule ya Msingi Tambukareli wawe watoto wazuri wenye nidhamu, wawatii na kuwaheshimu wazazi wao. Pia wayashike na kuyatendea kazi mawaidha waliyopewa kuhusu ukatili wa kijinsia ili kuisaidia serikali katika mapigano dhidi ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.