WANAFUNZI wa shule ya sekondari ya Viwandani iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kujengeana uwezo katika kujiamini na kusaidiana ili waweze kufaulu katika masomo yao ya kuwa raia wema pindi wamalizapo shule.
Rai hiyo ilitolewa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Viwandani katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Tunu Dachi alipofanya ziara ya kutembelea shule hiyo na kuongea na wanafunzi hao jana.
Dachi alisema “tumekuja kwenu kuwaletea elimu ya vitu vikubwa vitatu. Kwanza ni suala la lishe bora, pili elimu ya kujitambua na tatu elimu kuhusu ukatili wa kijinsia. Nafahamu shuleni hapa kuna wanafunzi ambao mnaonea wenzenu. Wanafunzi kuoneana ni tabia mbaya. Tabia hiyo ndiyo mwanzo wa ukatili wa kijinsia. Wanafunzi mnapofanyiwa uonevu huo toeni taarifa kwa mwalimu wa zamu au mwalimu wa darasa. Lazima mjijengee uwezo na tabia ya kujiamini siyo kuoneana wala kudharauriana”.
Aliwataka wanafunzi hao kusaidiana katika masomo ili waweze kufaulu katika masomo yao. “Nilipokuja mara ya mwisho hapa kuongea nanyi nilisisitiza upendo na kusaidiana. Wanafunzi wenye uwezo katika masomo kama hisabati jengeni tabia ya kuwasaidia wenzenu ambao wana uwezo mdogo katika hisabati, fanyeni hivyo hivyo na kwa masomo mengine. Wadogo zangu nawahakikishia kufanya hivyo wote mtafaulu katika masomo yenu na mwisho wa siku mtakuwa kuwa raia wema kwa Halmashauri yetu. Na huu ndiyo mwanzo wa uzalendo kwa nchi yenu” alisema Dachi.
Akitoa elimu ya umuhimu wa lishe bora kwa wanafunzi, Afisa Lishe katika Mradi wa Lishe Endelevu, Aloyce Peter kuwa lishe bora ni muhimu kwa ukuaji wa vijana. “Tunaposema kipindi cha ukuaji wa vijana ni miaka kati ya 10-19 kwa wavulana na wasichana. Hivyo, lishe bora ni vyakula ambavyo vinapatikana katika makundi matano ya vyakula na mchanganyiko wake ndio tunapata lishe bora au mlo kamili” alisema Peter.
Akiyataja makundi hayo ya vyakula na kazi zake alisema kuwa kundi la kwanza ni vyakula aina ya nafaka, mizizi pamoja na ndizi. Kazi yake ni kuupa mwili nguvu na nishati. “Kundi la pili ni vyakula asili ya wanyama na jamii ya mikunde. Kazi yake mwilini ni kuongeza madini chuma hasa kuwanufaisha watoto wa kike kuwasaidia kuongeza damu mwilini. Kwa vijana vinawasaidia kupata misuli na mwili mkubwa wenye nguvu. Kundi la tatu ni matunda. Matunda ya asili na ya kawaida tunayonunua sokoni. Matunda kazi yake ni kuimarisha kinga ya mwili na ufyonzaji wa vyakula tunavyokula” alisema Peter.
Akiongelea makundi mengine aliyataja kuwa ni vyakula vya mbogamboga ambavyo vinasaidia katika mmeng’enyo wa chakula na kuupa mwili madini mbalimbali. “Kundi la tano ni vyakula aina ya mafuta, sukari na asali. Vyakula hivi inashauriwa vitumike kwa kiasi kidogo kwa sababu vina nishati ya kutosha. Kama unakula mafuta mengi na sukari nyingi siyo mazuri mwilini. Sisi tupo katika kipindi cha ujana na katika kipindi hiki kuna ukuaji kupita kawaida, katika ukuaji huu lishe ni muhimu sana” alisema Peter.
MWISHO
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.