Na. Theresia Nkwanga, IYUMBU
Wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari Iyumbu wametakiwa kuwa na tabia nzuri, kushika mafundisho wanayopewa shuleni na nyumbani pia kuachana na mambo ya utandawazi sababu unasababisha mporomoko wa maadili.
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa Viti Maalum wa Jiji la Dodoma, Wendo Kutusha alipokuwa akiongea na wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari Iyumbu iliyopo Kata ya Iyumbu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kutusha alisema kuwa wanafunzi wanatakiwa kutii na kuheshimu mafundisho wanayopewa, kuacha kuiga mambo ya mitandaoni ambayo kwa kiasi kikubwa yanapelekea watoto kuharibikiwa na kushindwa kuzifikia ndoto zao. “Wewe ukiwa msichana ukaolewa na msichana mwenzako malengo yako yatatimia? utaweza kuwa mama? na kwa wavulana vilevile, mkioana wavulana kwa wavulana mtakuwa baba?, tuache kuiga mambo ya mitandaoni yanaharibu malengo yetu. Niwaombe watoto wangu wazuri muwatii wazazi wenu muwatii wakubwa wenu, ukifanya matendo mabaya mkubwa anapokuadhibu mwambie asante unanifundisha tabia njema. Acheni kuwatukana wakubwa wenu wanapowarekebisha sio tabia nzuri” alisema Kutusha.
Akiongelea kuhusu ukatili wakijinsia alisema kuwa kuporomoka kwa maadili kwenye jamii ni moja kati ya sababu kubwa inayosababisha vitendo vya ukatili wa kijinsia kuendelea kushamiri.
“Siku hizi watoto mnavaa nguo za hovyo zinazoonesha sehemu zenu za miili yenu hasa nyie wakike, mnasema mnaenda na fasheni mnatembea vitovu wazi hali inayopelekea kufanyiwa matendo ya ukatili wakijinsia. Mnapovaa nguo zinazoshawishi kuna wanaume wasio na maadili wanashawishika nakuanza kuwasumbua kimapenzi, wengine wanaenda mbali zaidi na kuwataka kinguvu huku wakiwapa vitisho” alisema Kutusha.
Aidha, alimshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mikopo isiyo na riba kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu. Mikopo hiyo imekuwa chachu katika kuwainua kiuchumi. “Mtu anapofanya kazi nzuri lazima tumpongeze, Rais wetu anatuheshimisha sasa tunatembea kifua mbele tunaachana na mikopo ya kausha damu. Hivyo, niwaombe wenzangu tuwe waaminifu turejeshe kwa wakati tusiporudisha tunasababisha wengine wanakosa mikopo. Jana tulikuwa nzughuni mkopo uliopita walipata milioni 50 ila sasa hivi wamepata milioni 300 kigezo kikubwa ni kurudisha kwa wakati”. alisema Kutusha.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.