Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameagiza wanafunzi wote ambao hawajaripoti shuleni watafutwe ili waweze kuripoti mapema na kuanza masomo akikemea vikali tabia ya wazazi kuwafundisha uvivu watoto wao.
Senyamule alitoa agizo hilo alipofanya kikao na kamati za maendeleo za kata nne ambazo wanafunzi waliopangiwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Viwandani wanatoka, kikao kilichofanyika shuleni hapo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa takwimu alizopata hadi jana zinaonesha kuwa shule ya sekondari Viwandani inaongoza kwa kuwa na kiwango kidogo cha wanafunzi kuripoti. “Wanaotakiwa kutafuta watoto hawa ni kamati za maendeleo za kata, wenyeviti wa mitaa na watendaji wa mitaa. Nilifahamishwa kuwa watoto wa shule ya sekondari Viwandani wanatoka katika kata nne ndiyo maana nikaitisha kikao na kamati za maendeleo za kata hizo ili tuweze kuulizana walipo watoto hao” alisema Senyamule.
Wakati huohuo, alipongeza ongezeko la watoto kuripoti ngazi ya mkoa hadi kufikia asilimia 78. “Niwapongeze kuwa watoto wameweza kuongezeka. Wiki iliyopita tulikuwa na asilimia 69 kimkoa ila mpaka jana tulikuwa na asilimia 78 kimkoa. Lakini bado asilimia 78 ni ndogo kuna kama asilimia 22 ambao hawajaripoti kwa kidato cha kwanza. Bado tunakazi kubwa ya kufanya. Tumieni mtandao wa watendaji ili wanafunzi watafutwe wote ambao hawajaripoti shule waweze kuripoti” alisema Senyamule.
Vilevile, alikemea tabia ya baadhi ya wazazi kuwafundisha Watoto wao uvivu. Alisema kuwa wapo baadhi ya wazazi ambao wanawaruhusu Watoto wao kuchelewa kuripoti shuleni kwa kisingizio kuwa masomo hayajaanza na hatimae kushindwa kwendana na kasi ya mwalimu.
Kwa upande wa Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Upendo Rweyemamu alisema kuwa changamoto moja wapo ni wazazi wanapohamisha wanafunzi kutoka shule ya sekondari viwandani hawatoi taarifa kwa uongozi wa shule huyo.
“Mheshimiwa mgeni rasmi, utaona shule ya sekondari Viwandani ina asilimia ya chini kabisa ya kiwango cha kuripoti, ina asilimia 42. Shule hii inalishwa na shule nne za msingi, shule tatu ni za binafsi na moja ya serikali. Wazazi wanapoamua kuwapeleka wanafunzi shule binafsi hawarudi kutoa taarifa kwa shule husika” alisema Rweyemamu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.