JAMII imeshauriwa kuchangamkia fursa zilizopo katika ufugaji wa samaki katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kujipatia kipato na kukabiliana na tatizo la lishe.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Uvuvi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Vestina Mahundi (pichani juu) alipokuwa akielezea fursa za ufugaji samaki ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika banda la mifugo kwenye maonesho ya Nanenane yanayoendela Nzuguni jijini hapa.
Mahundi alisema “katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, fursa zipo nyingi katika ufugaji wa samaki. Kwanza ufugaji samaki utamsaidia mfugaji kuuza na kupata fedha kwa ajili ya matumizi mbalimbali hivyo kuongeza kipato na kukuza uchumi wa Taifa. Lakini Dodoma ni Mkoa uliathirika na tatizo la udumavu. Kwa mujibu wa takwimu, tuna asilimia 31 ya udumavu katika Mkoa wetu wa Dodoma. Hivyo, tunahamasisha watu wafanye ufugaji wa samaki katika mabwawa au malambo ili kukabiliana na tatizo la udumavu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba samaki ana protini kwa wingi na lishe bora”.
Katika kufanikisha ufugaji wa samaki, alishauri watu wajiunge katika vikundi kuunganisha nguvu ili waweze kufanya ufugaji kibiashara na kupata tija zaidi kupitia ufugaji huo. “Katika Mkoa wa Dodoma tuna upungufu wa samaki. Hivyo, tunategemea samaki kutoka mikoa mingine ya Mwanza, Mara na Dar es Salaam. Utatuzi wa hili, Halmashauri inaendelea kutoa elimu na hamasa ili watu wengi washiriki katika ufugali samaki wa kisasa” alisema Mahundi.
Maonesho ya Nanenane mwaka 2020 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi chagua kiongozi bora”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.