Na. Dennis Gondwe, CHAMWINO
WANANCHI wa Kata ya Chamwino wametakiwa kuzingatia lishe bora ili kujikinga na udumavu na magonjwa ili wawe na afya njema itakayowawezesha kuzalisha mali.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mganga mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Situ Muhunzi alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Kata ya Chamwino waliojitokeza katika maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe iliyofanyika katika viwanja vya Wajenzi jijini Dodoma.
Muhunzi alisema “lishe bora ni muhimu kwa maisha ya mwanadamu. Awali Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alitueleza makundi matano ya ambayo ni Kundi la nafaka mizizi na ndizi mbichi, Kundi la Vyakula vya asili ya wanyama na jamii ya mikunde, Kundi la mbogamboga, Kundi la matunda, na Kundi la asali, sukari na mafuta. Kwa Mkoa wa Dodoma bado udumavu upo kwa asilimia 30.7 na miaka mitatu nyuma tulikuwa asilimia 37”.
Afya na lishe ni muhimu kwa wananchi wote, endeleeni kutumia kutuo cha kutolea huduma za Afya cha Chamwino ili kupata elimu ya lishe na huduma nyingine za afya na tiba. “Na leo hapa tumeleta huduma mbalimbali za kuchungaza hali ya lishe, virusi vya Ukimwi na kupata vitamin A kwa watoto na kufuatilia mapishi ya chakula lishe kilichokuwa kinaandaliwa hapa uwanjani” alisema.
Akiongelea afya na lishe, alisema kuwa vinaenda sambamba na ufanyaji wa mazoezi. “Mazoezi ni muhimu katika kujenga na kuboresha afya za wananchi wa Kata ya Chamwino na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ujumla. Mazoezi yanatukinga na magonjwa yasiyoambukiza ambayo yameibuka kwa wimbi kubwa katika siku hizi. Hivyo, ni muhimu kwa wananchi kufanya mazoezi kama ambavyo tumefanya leo” alisema Muhunzi.
Maadhimsiho ya Siku ya Afya na Lishe katika Kaya ya Chamwino yaliongozwa na kaulimbiu isemayo “Lishe bora kwa ustawi wa afya zetu na maendeleo ya kata yetu”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.