Na. Dennis Gondwe, MSALATO
WANANCHI wa Kata ya Msalato iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamemshukuru Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea shule mpya na kuwapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Shukrani hizo zilitolewa na Afisa Mtendaji Kata ya Msalato, Devotha Selufara alipokuwa akiwatambulisha wataalam wa kata yake katika Shule ya Msingi Chikole kwa mgeni rasmi Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Mkoa wa Dodoma.
Selufara alisema “Shule ya Msingi Chikole ina wanafunzi 790 ilianza mwaka jana mwezi Julai. Baada ya kumaliza ujenzi ulioanza mwezi Aprili, 2023 kwa fedha ya mama Samia Suluhu Hassan aliyotupatia shilingi 318,800,000 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi Chikole, ambapo tulijenga madarasa tisa, matundu 16 ya vyoo, jengo la utawala moja, tumefanikiwa kujenga madarasa ya chekechea ya mfano ni kama shule za mchepuo wa kiingereza pamoja na madawati yanayotosheleza madarasa yote. Cha kufurahisha zaidi serikali yake imetujengea kisima cha maji chenye thamani ya shilingi 22,500,000, hivyo shule hii ni mahali salama kabisa kwa watoto wetu.
Kwa kuwa umefika hapa kiongozi wetu mkubwa wa kimkoa tunaomba utufikishie salamu sisi wananchi wa Kata ya Msalato za pongezi kwa kuweza kutukumbuka kutujengea shule hii na kuwapunguzia wanafunzi wetu kutembea mwendo mrefu”.
Aliongeza kuwa Rais, Dkt. Samia alitoa fedha shilingi 680,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa saba, mabweni manne na vyoo vyenye matundu 10 katika Shule ya Sekondari ya wasichana Msalato. “Mheshimiwa mgeni rasmi, mama huyu hakuishia hapo, alitupatia fedha shilingi 437,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi Msalato pamoja na madawati yake. Ambapo tulijenga madarasa 12, matundu 12 ya vyoo, ofisi mbili za walimu pamoja na eneo la kunawia mikono” alisema Selufara.
Afisa mtendaji huyo aliongeza kuwa walianza kujenga kituo cha afya kwa nguvu za wananchi zenye thamani ya shilingi 50,000,000 hadi usawa wa lenta. “Serikali ya mama Samia imetupatia fedha shilingi 30,000,000 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kituo hicho cha afya. Tunamshukuru sana mama yetu. Vilevile, tumejenga zizi la ng’ombe kwa shilingi 19,800,000. Kwenye Kata hii ya Msalato. Rais mama Samia ametoa karibia shilingi bilioni 1.3 kwa mwaka wa fedha 2023/2024” alisema Selufara.
Akiongelea zawadi za unga wa mahindi, maji, kalamu, na taulo za kike kwa shule za Kata ya Msalato alisema ni michango ya wananchi wa Msalato. “Hii ni michango ambayo tumeshiriki pamoja wanaume na wanawake tumeona tuadhimishe na ninyi watoto wetu wa shule za msingi na sekondari. Tunawashukuru wote walioguswa afya njema” alisema Selufara.
Maadhimisho ya siku ya wanawake Kata ya Msalato yalifanyika kwa kutoa elimu ya lishe bora kwa wanawake na hamasa ya kujishughulisha yakifanyika katika Zahanati ya Msalato inayozungukwa na mitaa sita ikikadiriwa kuhudumia watu 11,000.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.