Na. Dennis Gondwe, Makutopora
WANANCHI wa Kata ya Makutopora wametakiwa kuwajibika katika kurejesha mikopo ya asilimia 10 ya bila riba inayotolewa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa wajasiriamali kwa lengo la kuwainua kiuchumi.
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa Viti maalum Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Frola Liacho alipokuwa akiongea na wananchi wa Kata ya Makutopora iliyopo jijini hapa.
“Hakuna binadamu anayeishi bila kujishughulisha. Utafanya kazi utafanya biashara, utalima ili upate riziki na kuishi. Niongelee suala la mikopo. Kina mama, vijana na watu wenye mahitaji maalum wamenufaika. Kwa sasa suala hilo limesitishwa kwa muda ila baadae itarejeshwa. Nimekuja hapa kuhimiza urejeshaji wa mikopo baada ya kukopa. Hizi ni kodi zetu wenyewe tunakopeshana wenyewe ili kuweza kuinua vipato. Unapokopa zingatia urejeshaji ili uongezewe mkopo na mwingine apate mkopo” alisema Liacho.
Alisema kuwa vipo vikundi ambavyo vinasumbua kufanya marejesho. “Ndugu zangu mkutano huu utumike kuelimishana na baada ya hapa elimu hii muipeleke kwa ambao hawapo. Mikopo ndiyo inayotufanya kuongeza mitaji na kuishi vizuri. Ukichukua mkopo jitahidi upeleke kwenye malengo uliyokusudia. Kina mama wenzangu usichukue mkopo na kuona Mheshimiwa Zollo kavaa gauni zuri ukasema kile kitenge lazima na mimi nikakitafute, hatuwezi kufika. Chukua mkopo peleka kwenye malengo uliyokusudia” alisema Liacho.
Madiwani 14 wa Viti maalum wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wanafanya ziara katika kata 41 za jiji hilo kutoa elimu dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii na fursa za kiuchumi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.