WANANCHI 34 wa kata ya Mtumba ambao hawakuwepo wakati wa uthamini watalipwa fidia za ardhi yao na Halmashauri ya Jiji la Dodoma mwishoni mwa mwezi huu wa nane 2020.
Hayo yalisemwa jana na mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipokuwa akijibu swali la mwananchi wa Kata ya Mtumba, Jackson Seganje aliyetaka kujua malipo ya fidia kwa wananchi 34 ambao hawakuwepo katika uthamini uliopita wa eneo la Mtumba. Mafuru alisisitiza kuwa malipo hayo yatalipwa mwisho wa mwezi Agosti mwaka huu.
Mafuru ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Mipango miji, Ardhi na Maliasili katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema “Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, ni kweli kuna wananchi 34 ambao kwenye eneo tulilotwaa hawakuwepo wakati wa zoezi la uthamini. Eneo ambalo tulitwaa tulirudia mara nne zoezi la uthamini. Hii ni kwa sababu mnaweza kufanya zoezi hilo lakini bahati mbaya wachache wasiwepo wakati wa utekelezaji zoezi hilo, kuna kitu kinaitwa ‘supplementary valuation’ kwamba watakapokuwa wale watu tutawafanyia kitabu cha pili ili wa kwanza wanalipwa kwanza na wale wengine wanalipwa baadae. Sasa hawa waliobaki wananchi 34 ni wa awamu ya tano ambapo wanadai shilingi milioni 210” alisema Mafuru.
Mkuu huyo wa Idara alikiri kuwa wananchi hao walipaswa kulipwa mwaka wa fedha ulioisha ila taratibu hazikukamilika na kuahidi malipo hayo kufanyika kufikia mwisho wa mwezi Agosti, 2020. “Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ninachoweza kukuahidi pamoja na wananchi hawa ni kwamba kabla ya mwezi huu Agosti kuisha fedha zao zitakuwa kwenye akaunti zao. Malipo haya ni kipaumbele kwetu kwa sababu tulifunga nayo mwaka wa fedha uliopita” alisema Mafuru kwa kujiamini.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini (wa pili kutoka kulia waliokaa) akimsikiliza kwa makini Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji Joseph Mafuru (aliyesimama mbele) wakati akijibu swali la mwananchi wa Mtumba (hawapo pichani) kuhusu fidia ya wananchi wa eneo hilo. Wengine pichani, kushoto ni David Msasa Afisa Tarafa wa Kikombo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo kata ya Mtumba Nathanael Mlunya (wa tatu kulia waliokaa mbele) na Dionis Samo (wa kwanza kulia mbele) ambaye ni Mtendaji wa Kata ya Mtumba.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.