WANANCHI wa Kijiji cha Ilindi, Kata ya Ilindi katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, wametakiwa kutunza chakula baada ya kupata mavuno kuepuka kupata upungufu wa chakula kufuatia mvua nyingi kunyesha kwenye kipindi cha msimu wa kilimo mwaka huu.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule wakati alipofanya Mkutano wa hadhara na Wananchi wa Kata hiyo kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Ilindi.
Suala la utunzaji wa chakula limesisitizwa kwa kuzingatia juhudi za Rais Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwekezwa fedha nyingi kwenye kilimo.
"Serikali yetu imewekeza kujenga mabwawa ya umwagiliaji ili kuimarisha Kilimo. Nitoe msisitizo, tutunze chakula cha kutosha kutokana na mvua nyingi zilizonyesha mwaka huu. Tunza chakula unapovuna, uza ziada. Haitaleta sura nzuri kusikia munahitaji chakula baada ya kumalizika msimu huu wa Kilimo" Amesisitiza Mhe. Senyamule.
Aidha, msisitizo huo umefuatia kero mbalimbali zilizowasilishwa mbele yake ambazo zinaikabili Kata hiyo na zimepatiwa majawabu kutoka kwa wataalamu walioambatana na Mkuu wa Mkoa.
Awali, Mkuu wa Mkoa alikagua mradi wa vyumba viwili vya Madarasa na Ofisi moja ambao umeshakamilika na unatumika kwa Sasa kwenye shule hiyo na umegharimu Shilingi Milioni 40 zenye mchanganuo wa; Milioni 2.5 kutoka kwenye mapato ya ndani, Milioni 2.5 nguvu za wananchi na Milioni 35 kutoka Serikali kuu kupitia Mradi wa SEQUIP.
Mradi huo umesaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani kwani Sasa wanaweza kukaa kwa nafasi tofauti na awali hali inayopelekea kupata nafasi ya kusoma pasi na bughudha.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.