Na. John Masanja, DODOMA
Wananchi wa Dodoma wametakiwa kukemea na kuondokana na tabia za ukatili wa kijinsia unaofanyika ndani ya jamii wanazoishi ili kuandaa jamii iliyobora na yenye maendeleo kwa taifa.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alipokuwa akizungumza na hadhira katika Kongamano la kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, lililofanyika katika ukumbi mikutano wa 'Dear Mama' jijini Dodoma.
Aidha, Senyamule alizitaja takwimu za mwenendo wa matukio ya ukatili mkoani Dodoma, alisema kuwa kwa Mwaka 2023 (Januari - Agosti) matukio yaliyoripotiwa yalikuwa 3,012 huku watoto wakiwa ni 846 na watu wazima ni 2,166. Pia alisema kwa Mwaka 2024 (Januari - Agosti) matukio yamepungua hadi kufikia 2,352 huku watoto wakiwa 529 na watu wazima wakiwa 1,723.
Sambamba na hilo, Senyamule alitoa rai kuwa jamii iendelee kuelimishwa kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia na kuwataka wananchi kutosita kutoa ushirikiano endapo kuna viashiria au ufanyikaji wa vitendo vya ukatili ili hatua stahiki zichukuliwe kwa watakaobainika.
"Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa akifanya jitihada kubwa katika kutokomeza ukatili wa kijinsia, amefanya mambo mengi baadhi yake ni ujenzi wa Shule zakutosha, utoaji wa mikopo kwa wanawake, urahisishaji wa huduma kama ya upatikanaji wa maji pamoja na uwepo wa nishati safi. Hayo yote ukiyatazama Kwa undani, yamechangia kwa sehemu kubwa kupunguza matatizo hayo ya ukatili wa kijinsia" alisema Senyamule.
Senyamule alisema yupo tayari kutoa msaada na ushirikiano kwa yeyote atakayetoa taarifa katika ofisi yake kuhusu utendekaji wa matukio ya kikatili ya kijinsia.
"kila mmoja akatimize wajibu wake kwa kuhakikisha hakuna tendo la kikatili linalotendeka mbele yake, kwa kufanya hivyo tutaikomboa Dodoma" alisema Senyamule.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma SACP. George Katabazi, alisema Jeshi la polisi limeendelea kupambana dhidi ya matendo ya ukatili wa kijinsia na kwa kupitia siku 16 za kampeni ya kutokomeza ukatili wa kijisia, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limefanya shuguli kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia dawati la jinsia na kufanya matendo ya huruma kwa wahitaji na waathirika wa matendo ya kikatili.
Vile vile, Kamanda Katabazi, alisema Jeshi la Polisi halitaacha kuchukua hatua kwa yeyote atakaefanya vitendo vya ukatili na hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
"Kwa pamoja niwaombe wananchi tushirikiane kutokomeza ukatili wa kijinsia ndani ya jamii zetu kwa ustawi na maendeleo ya taifa letu" alisema Kamanda Katabazi.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Alhaj. Jabir Shekimweri, aliwataka wananchi kuepukana na mila potofu zinazipelekea kutendeka kwa matendo ya ukatili ndani ya jamii na kuwataka wananchi kuwa na hofu ya Mungu ili kuepukana na vitendo hivyo.
Aidha, Shekimweri aliwataka wananchi kutumia muda wao katika siku hii ya kilele cha maadhimisho ya kupinga ukatili wa kijinsia, kujitafakari na kubaini sababu zingine zinazopelekea matendo hayo na alitoa rai kwao kuyaacha mara moja.
"Niwapongeze na kuwashukuru wadau mbalimbali wanaoisaidia Serikali katika kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia, kiukweli mnafanya kazi nzuri sana na msiache kufanya hivyo" alisema Shekimweri.
Akitamatisha salamu zake, Shekimweri alimshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada anazozifanya katika kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Sambamba na hilo alitoa kongole kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma SACP George Katabazi, kwa namna nzuri ya uongozi wake unaoleta manufaa mkoani Dodoma.
Ikumbukwe kuwa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia hufanyika kuanzia tarehe 25 Novemba hadi tarehe 10 Desemba kila mwaka, kwa mwaka 2024 maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yameongozwa na kauli mbiu inayosema “Kuelekea Miaka 30 ya Beijing: CHAGUA Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.