MFUKO wa Afya ya Jamii iliyoboreshwa (CHF) ni mkombozi wa wananchi wa Mtaa wa Kawawa, Kata ya Mbalawala kwa sababu unawahakikishia uhakika wa matibabu wanapougua.
Kauli hiyo ilitolewa na mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Revocatus Baltazary alipokuwa akiongea na wananchi wa Mtaa wa Kawawa jijini Dodoma kwenye mkutano wa hadhara wa Mtaa huo.
Dkt. Baltazary alisema kuwa CHF iliyoboreshwa inalipiwa shilingi 30,000 tu kwa mwaka. “Ndugu zangu, CHF iliyoboreshwa ni muhimu sana kwa sababu unapolipia shilingi 30,000 watu sita katika kaya yako wanapata matibabu bure kwa mwaka mzima. Wote tunafahamu kuwa ugonjwa huwa haupigi hodi. Hivyo, maandalizi ya mapema ni muhimu sana hasa kipindi ukiwa mzima” alisema Dkt. Baltazary kwa msisitizo.
Aidha, aliwataka viongozi wa Mtaa kujiunga na mfuko huo ili wawe mfano kwa wengine wanaowaongoza. “Ndugu viongozi mnawajibu wa kuwahamasisha wananchi wengi wajiunge na CHF iliyoboreshwa kwa kuwaelezea faida zake kabla hawajaugua” alisema Dkt. Baltazary.
Wakati huohuo, aliwataka wakina mama kuhudhuria kliniki wanapojigundua kuwa wajawazito mapema. Alisema kuwa hudhurio la mapema na vipimo atakavyofanyiwa mama mjamzito vitamsaidia kutohatarisha ujauzito wake. Alisema kuwa katika kipindi hicho mama wajawazito hupewa madini ya ‘folic acid’ yanayosaidia wakati wa kuumbwa kwa mtoto ili asiwe na kichwa kikubwa na mgongo wazi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.