Afisa Afya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Abdallah Mahia amewataka wananchi kuzingatia kanuni za afya kwa waandaji wa vyakula majumbani na hata wauzaji wa vyakula na vinywaji, kuzingatia matumizi ya vifaa kinga (sare za kazi - 'uniform') ili kuweza kuzuia magonywa ya kuambukiza.
Mahia ameyasema hayo leo katika kituo cha Radio cha Dodoma FM kwenye kipindi cha 'Dodoma live' alipokuwa anaeleza kuhusiana na maambukizi ya sumu inayosababishwa na kuchafuka kwa chakula, maji au kinywaji kutokana na bakteria na vimelea mbalimbali jambo ambalo limekuwa likihatarisha maisha ya watu na kusababisha madhara endapo mtu atakula chakula hicho.
Mahia alieleza vihatarishi vinavyoweza kusababisha maambukizi kwenye chakula, ambapo aliyataja baadhi ya maeneo ambayo ni hatarishi zaidi na yanahitaji umakini mkubwa katika uandaaji wa chakula.
“Maambukizi kwenye chakula hutokea zaidi katika vyakula vilivyoandaliwa katika misiba, kazini, matanga, hitma, ngoma, harusi na mikusanyiko inayohusisha ulaji wa chakula kwa pamoja ambapo mtu mmoja au kundi la watu hupata ugonjwa kutokana na kutozingatia kanuni za afya.
“Watoto wadogo pamoja na wazee ni makundi ambayo yanaathiriwa zaidi kutokana na kinga zao kuwa chini, wanapopata bakteria mwili unashindwa kupambana navyo, pamoja na watu wenye matatizo ya kiafya, magonjwa ya figo na kisukari, wenye upungufu wa kinga mwilini, na wasafiri wanaotembelea maeneo yanayojulikana kuwa na vimelea vinavyosababisha hali hii kwa wingi,” alisema Mahia.
Afisa afya huyo alifafanua juu ya dalili za mtu ambaye tayari ameathiriwa na sumu kwenye chakula pamoja na kuelekeza madhara yatokanayo na ugonjwa huo.
“Vimelea vya sumu huingia kwenye chakula wakati wa maandalizi na upikaji mbaya, utumiaji wa maji yasiyo salama yenye vimelea vya kinyesi, mikono pamoja na vyombo vikiwa vichafu, kachumbari isiyoandaliwa kwa usafi, matunda yasiyooshwa na mboga za majani zisipoiva vizuri, nyama isipoiva vizuri, na mayai mabichi.
“Dalili za mtu mwenye maambukizi kwenye chakula ni maumivu ya tumbo, homa na kujihisi baridi, kuumwa kichwa, kichefuchefu na kutapika, kuharisha majimaji au damu, mwili kuwa dhaifu na ulegevu unaosababisha mtu kushindwa kupumua na hatimaye husababisha kifo.
“Madhara hutegemea na aina ya bakteria anayesababisha ugonjwa huu, lakini mengi huwa ni kupata matatizo ya figo, kutokwa na damu bila kukoma, magonjwa ya viungo ya mwili, magonjwa ya mfumo wa fahamu na madhara katika moyo,” aliongeza Afisa Afya.
Aidha, alisema visababishi vinavyosababishwa na maambukizi kwenye chakula ni pamoja na vimelea vya bacteria na virusi ambapo alisisitiza juu ya kuhakikisha kunawa kwa maji ya moto na sabuni mara baada ya kutoka chooni, na baada ya kutoka, kumnawisha mtoto anapokuwa amejisaidia na kusisitiza suala la usafi kuzingatiwa jijini kote.
Pia amesisitiza wananchi hasa katika kipindi cha mvua kuhakikisha wanazingatia matumizi sahihi ya vyoo, kuepuka kujisaidia kwenye vyanzo vya maji na kuepuka kutiririsha au kufungulia vyoo kuelekea kwenye maji ya mvua. Mahia amesisitiza katika Jiji la Dodoma magonjwa ya kuambukizwa ni historia hivyo ametoa onyo kwa yeyote atayekaidi taratibu za afya, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.