Mratibu wa Bima ya Afya ya Jamii ya CHF Iliyoboreshwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Patrick Sebiga amezungumzia changamoto wanazokutana nazo katika zoezi la kuwahamasisha Wananchi kujiunga na Bima hiyo, huku changamoto kubwa ikiwa ni uelewa wa Wananchi juu ya Bima hiyo hasa urahisi wa upatikanaji wake kwamba sio jambo la kawaida kutibiwa watu sita kwa gharama ya shilingi elfu thelathini kwa Mwaka mzima.
Sebiga ameyasema hayo leo ofisini kwake alipokua akizungumzia mafanikio waliyoyapata katika Maonesho ya Wakulima ya Nanenane 2020 ambayo kwa Kanda ya Kati yalifanyika Jijini Dodoma.
Amesema kuwa idadi ya wananchi wanaofika katika ofisi zao ili kukata Bima hiyo imeongezeka baada ya kumalizika kwa Maonesho ya Nanenane jambo ambalo linaonesha mapokeo mazuri ya CHF iliyoboreshwa, licha ya Wananchi walio wengi kuhofia upatikanaji wa huduma Bora katika Vituo vya Afya ukilinganisha na bei ya Bima hiyo.
”Changamoto kubwa tunayokutana nayo ni Watu kutoamini kwamba shilingi elfu thelathini inaweza kutibu watu sita kwa mwaka mzima na wote wakapata huduma nzuri, ila niwahakikishie Watanzania hasa wa Dodoma kuwa Bima hii imeletwa ili kumkomboa mtu wa chini, kwa hiyo wajiunge na wawaulize wale wenye Bima hizi kuhusu huduma wanazopata watapata majibu” Alisema Sebiga.
Aidha, Sebiga aliwashukuru Wananchi wanaoendelea kuwa mabalozi wazuri wa Bima hiyo jambo ambalo linafanya idadi ya walioandikishwa kuwa kubwa kwani kwa kufanya hivyo wanaokoa idadi kubwa ya Watanzania ambao wangeweza kupoteza maisha kutokana na uwepo wa gharama kubwa za matibabu.
Pia amewashukuru wafanyakazi wenzake ambao walishirikiana kwa pamoja na kuhakikisha idadi kubwa ya wananchi waliotembelea katika Maonesho ya Nanenane wanapata Bima hizo jambo lililopelekea Mfuko huo wa Bima ya CHF iliyoboreshwa kushika nafasi ya pili kwenye maonesho hayo kwa upande wa Sekta zinazotoa Bima za Matibabu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.