WAKAZI wa Jiji la Dodoma wameshauriwa kufikisha kero na malalamiko yao mbalimbali yanayohusu huduma zinatolewa na Halmashauri katika Ofisi za Kata na Mitaa badala ya kwenda moja kwa moja Ofisi Kuu za Jiji ili kuokoa muda na gharama kwani Mfumo wa Serikali unaanzia kwenye ngazi ya Mtaa au Kijiji.
Ushauri huo umetolewa na Ofisa Malalamiko katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma Gisela Mmavele alipokuwa akitoa elimu ya upokeaji na ushughulikiaji wa malalamiko ya Wananchi katika kipindi cha ‘Dodoma live mtaani’ kinachorushwa na kituo cha redio Dodoma FM jana ofisini kwake.
Ofisa huyo alishauri Wananchi wanaokuwa na malalamiko ya kiutendaji na huduma zinazotolewa katika maeneo yao kuanzia kuwasilisha malalamiko hayo kwa Watendaji wa maeneo yao ili yaweze kushughulikiwa mapema hali itakayoboresha zaidi ushughulikiaji wa malalamiko kwa wakati.
“Yapo malalamiko ambayo utatuzi wake upo katika ngazi ya Mtaa na Kata, kitendo cha mwananchi kufunga safari kuja Makao Makuu ya Halmashauri kinampotezea muda mwingi na kumuongezea gharama” alisema Mmavele.
Mmavele alisema kuwa katika kuhakikisha wananchi wanahudumiwa vizuri na kuondoa kero zitokanazo na utolewaji wa huduma katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, yupo Ofisa maalum kwa ajili ya kupokea, kuratibu na kushughulikia malalamiko ya wananchi.
“Malalamiko hayo hupokelewa, husikilizwa, na kutatuliwa katika hali ya usiri mkubwa”, aliongeza.
“Tumekula kiapo cha kutunza siri, hivyo huwezi kukuta taarifa ya malalamiko yaliyowasilishwa sehemu isiyotakiwa…na tumekuwa na utaratibu mzuri wa utoaji majibu kwa wale wote wanaowasilisha malalamiko yao kwetu” alisisitiza Mmavele.
Halmashauri ya jiji la Dodoma imeanza utaratibu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu uwepo wa Kitengo cha kupokea, kusikiliza, na kutatua malalamiko ya Wananchi ili kuondoa manung’uniko katika jamii na kuwahakikishia wananchi huduma bora.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.