BAADHI ya Wakazi wa Manispaa ya Dodoma wameunga mkono zoezi la kubomoa nyumba na vibanda vilivyojengwa katika maeneo yasiyo rasmi ikiwemo hifadhi za barabara, maeneo ya wazi, na wale waliojenga katika viwanja wasivyovimiliki kihalali linalofanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.
Baadhi ya wananchi waliotoa maoni yao katika maeneo ya Kisasa, Majengo, Nkuhungu, na Kikuyu ambapo zoezi hilo lilitekelezwa hapo jana, wamesema kumekuwapo na mazoea ya watu kuvamia maeneo yasiyo rasmi na kuanzisha makazi au vibanda vya biashara jambo linaloharibu taswira ya Mji.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo la siku mbili lililoanza jana, Afisa Mdhibiti Ujenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Ally Bellah alisema zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa sheria na kwamba taratibu zote zimefuatwa kabla ya kufikia hatua ya uvunjaji.
“Maeneo yote haya tunayovunja wahusika walishapewa notisi kwa mujibu wa Sheria lakini wengi wao wamekaidi…kwa wale waliostahili kupewa fidia walishapewa fidia zao muda mrefu” alisema.
Bellah ametoa wito kwa Wakazi wote wa Manispaa na hata wageni wanaohamia kuepuka kununua ardhi kienyeji kwani wanaweza kutapeliwa na kuuziwa maeneo ya wazi au yasiyo ya makazi na kujikuta wakipata usumbufu usio wa lazima.
“Hata wageni wanaohamia Manispaa ya Dodoma niseme kwamba tunawapenda sana na tunawakaribisha ila watakapohitaji ardhi au viwanja kwa ajili ya kujenga wahakikishe wanawasiliana na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ili wawe salama” alisisitiza.
Alisema Mji wa Dodoma ni Makao Makuu ya Nchi hivyo lazima uwe na muonekano wa kuvutia na kwamba zoezi la bomoa bomoa ni endelevu ili kudhibiti ujenzi holela na kusimamia ujenzi bora kwa mujibu wa vibali vinavyotolewa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.