Spika msaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda amewataka wanawake nchini kuacha woga wakati wa mapambano ya kutafuta fursa mbalimbali za kielimu, uchumi na siasa vinginevyo masuala ya usawa wa kijinsia itabaki kuwa ndoto.
Makinda amesema hayo jana jijini Dodoma katika Kongamano la Uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambalo pamoja na mambo mengine limejadili utekelezaji wa maazimio ya ulingo wa Beijing yaliyowekwa miaka 25 iliyopita.
Amesema wanawake nchini Tanzania ni zaidi ya asilimia 51 ya wananchi wote hivyo kundi hili lina uwezo kufikia maamuzi yenye tija kwa wanawake lakini tatizo kubwa ni woga wa kuthubutu ilhali uwezo wanao.
“Wanawake acheni woga na unyonge maana wanawake ambao ni wawakilishi wa majimbo wameendelea kuaminika na kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa amesema.
Ameongeza kuwa, jitihada zinaonekana ingawa zinasuasua sana hasa kwenye mambo ya siasa.
Hatuwezi kusema tuna usawa wa kijinsia wakati bado hatujaweza kuchaguliwa na watu. Kama isingekuwa kipengele cha viti maalum, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lingekuwa na wanawake asilimia 6 tu, idadi ambayo ni ndogo sana”
Ameongeza kuwa asilimia 30 ya wabunge wa viti maalum na wale wa kuteuliwa haina mantiki katika kuelekea usawa wa kijinsia.
Amewahimiza wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi hasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2020.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema mchango wa viongozi wanawake wakiwemo wastaafu umeleta mabadiliko makubwa katika kuelekea maendeleo jumuishi.
Waziri Mwalimu amemtaja Mama Makinda kuwa kioo kwake wakati wa kutekeleza majukumu yake katika Wizara huku akiwapongeza wanawake walioshiriki katika harakati za kuelekea ukombozi wa mwanamke maarufu kama Mkutano wa BEIJING.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akiwasilisha utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Beijing amesema mambo mengi yamefanyika ikiwemo kuwezesha wanawake kiuchumi kupitia mifuko ya uwezeshwaji kiuchumi.
Dkt. Jingu amesema kwa kipindi cha miaka minne, zaidi ya shilingi bilioni 39 zimetolewa kwa wanawake zaidi ya laki 8 kupitia asilimia 10 ya fedha za ndani za Halmashauri na shilingi bilioni 2 zimetolewa kwa zaidi ya wanawake elfu 3 kupitia dirisha la wanawake la Benki ya Posta Tanzania mwezi Agosti 2018 hadi Machi 2019.
Ameongeza pia kuwa, umiliki wa ardhi umeongezeka kwa wanawake kutoka asilimia 6 mwaka 2014 hadi 16 mwaka 2017 pamoja na ushiriki wa wanawake katika maonesho ya Biashara ya kimataifa kutoka 1183 mwaka 2017 hadi 13016 mwezi Machi mwaka 2019.
Kongamano hilo la siku moja limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wadau wa afya na wanafunzi kutoka shule za Sekondari zilizopo mkoani Dodoma.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akiongea katika kongamano hilo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akiwasilisha utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Beijing mbele ya wajumbe wa kongamano ili kujadili utekelezaji wa maazimio ya ulingo wa Beijing yaliyowekwa miaka 25 iliyopita.
Kongamano la siku moja limehudhuriwa pia na wanafunzi kutoka shule za Sekondari za mkoa wa Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.