WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa taasisi za wanawake zilizosajiliwa kuchangamkia fursa ya mikopo kupitia madirisha mbalimbali.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Taasisi ya CITIZENS FOUNDATION uliofanyika mkoani Dar Es Salaam Januari 06, 2024.
Amesema kwamba uwezeshaji wanawake ni jukumu la Serikali kwa kushirikiana na wadau wote wenye mapenzi mema, hivyo taasisi hiyo na nyingine zitaongozwa kama wanawake wengine katika kuwezeshwa.
Waziri Dkt. Gwajima ameeleza kwamba Serikali ipo tayari kushirikiana na taasisi hiyo kwa sababu moja ya mikakati iliyojiwekea ni kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake nchi nzima ili wajikwamue kiuchumi na kuachana na utegemezi sambamba na kuwatafutia fursa za kupata mikopo bila riba au yenye riba nafuu.
"Aidha, kama tunavyojifunza kwenye programu mbalimbali za wanawake, hata kwenye programu zenu ikiwemo WOPEC (WOMEN POVERTY ERADICATION CAMPAIGN) pia tutafanya hivyo na kuwashauri." amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwaasa wanawake wa taasisi hiyo na nchini kote kusimama imara kwenye safari ya maendeleo ya kiuchumi pasipo kuyumbishwa na nyakati zozote na wanapohitaji ufafanuzi wawasiliane na Wizara yao ya jamii kwa ushirikiano dhidi ya changamoto kwenye safari ya maendeleo.
Ameipongeza taasisi hiyo kwa miradi inayowezesha watoto na wanawake ya MTOTO NI MAMA INITIATIVE, programu ya LEGAL CLINIC ya msaada wa kisheria na kampeni ya kutokomeza umaskini kwa wanawake Tanzania ya WOPEC.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Lilian Wasira amebainisha kwamba taasisi imefanikisha kusomeshwa kwa watoto 100 wanaoishi kwenye mazingira magumu kupitia mradi wa MTOTO NI MAMA INITIATIVE. Ameongeza kuwa, waligundua umaskini ndio chanzo cha ukatili wa kijinsia na watoto hivyo wakaona mbinu ni kuwakwamua wanawake kiuchumi kupitia mradi wa kuwainua wanawake uitwao WOPEC.
Baadhi ya wanachama wa taasisi hiyo wakizungumza katika mkutano huo wameiomba Serikali kuwashika mkono na kuhakikiaha wanajikwamua kiuchumi ili wainue familia zao hasa watoto.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.