Na. Faraja Mbise, DODOMA
WANAWAKE wameshauriwa kutumia nishati safi ya kupikia katika kuandaa vyakula vya watoto kwasababu upatikanaji wake ni rahisi ukilinganisha na matumizi ya nishati chafu ya kupikia kama vile mkaa na kuni kutokana na kuwa inaokoa muda na ni salama kwa mazingira.
Ushauri huo ulitolewa na Afisa Lishe wa Kituo cha Afya cha Makole, Frida Mollel wakati akiwafundisha juu ya jiko darasa kwa akina mama wanaonyonyesha waliohudhuria kliniki katika Kituo cha Afya Makole kilichopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mollel aliwataka kutumia nishati safi ya kupikia wanapoandaa chakula cha watoto wao kwasababu upatikanaji wake ni rahisi na usalama kwa mtoto ni mkubwa zaidi ukilinganisha na matumizi ya nishati chafu ya kupikia. “Sambamba na elimu ambayo tumeitoa, utumiaji wa nishati safi umekuwa ukirahisisha uandaaji wa vyakula, ambayo inatoa usalama wa mtoto. Kwa mfano, mama ambaye atapika kwa kutumia gesi, uji wake ataweza kuusimamia na kusubiri kwasababu ule uji utaiva kwa haraka lakini kwa mama ambaye anatumia mkaa, itabidi atumie kwa muda mrefu, muda mwingine anaweza kujisahau na mtoto akaungua. Lakini pia tumeona matukio ya watoto kuungua kwa moto yamepungua kwasababu ya nishati safi” alisema Mollel.
Akiongelea uandaaji wa chakula, alisema kuwa ni muhimu kuzingatia makundi yote ya chakula na kuachana na mfumo uliopo wa kuandaa kundi moja tu la chakula. “Tamaduni zetu za kiafrika tumekuwa tukiandaa aina moja ya chakula kwa watoto, ambayo tukiangalia kwenye taarifa ya Digital Health Incentive Scheme (DHIS) inaonesha kwamba tuna ‘low food diversification’ kwa watoto ambayo inatupelekea kwa ‘indicator’ hiyo kuwa chini sana. Kwahiyo, mafunzo haya ya jiko darasa yameweza kuwasaidia akina mama kutumia makundi mengi ya vyakula kwa wakati mmoja na kuhama kutoka kutumia kundi moja la wanga kwa wingi kwenye vyakula kama kutumia aina ya mizizi na wanga. Kinamama kama mnavyojua walikuwa na kawaida ya kuandaa unga wa lishe ambapo wanaweka mahindi, mchele na vitu vingine ambavyo si afya nzuri kwa watoto kwasababu havitoi virutubisho vinavyohitajika kwa watoto” alisisitiza Mollel.
Kwa upande wake, mtoa huduma ya unyonyeshaji sahihi kwa watoto wachanga katika Kituo cha Afya Makole, Sylivia Kitalo alitoa ushauri kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia, namna inavyowasaidia akina mama wanaonyonyesha na kutaja madhara ya kutumia nishati chafu ya kupikia kama mkaa na kuni. “Nishati safi ya kupikia ni nzuri na tunamshukuru Rais wa nchi yetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea nishati safi ya kupikia, zinaweka mji safi, miti inakuwa ya kutosha kama haijakatwa. Ninawashauri kina mama ambao bado wanatumia nishati chafu ya kupikia, ninawaomba waepukane nayo na waanze kutumia nishati safi ya kupikia ambayo ni umeme na gasi” alisema Kitalo.
Nae mnufaika wa elimu ya jiko darasa, Esther Samwel alielezea namna ambavyo elimu kupitia jiko darasa ilivyomsaidia kuandaa lishe bora na alielezea umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia na usalama wake kwa mazingira ya mtoto. “Nimekutana na darasa zuri ambalo limenisaidia kuelewa kwa baadhi ya vitu na pia nimejifunza namna ya kuandaa vyakula kwa ajili ya watoto, hata sisi wajawazito na kutengeneza lishe bora kwa ajili ya watoto wetu. Tumejifunza kutumia nishati bora ya kupikia. Sio lazima tutumie mikaa au kuni kwasababu inaharibu hali ya hewa. Kwahiyo, ni vizuri akina mama majumbani tujitahidi kutumia nishati bora na inatusaidia kuwahi kupika kwa haraka” alieleza Samwel.
Vilevile, mkazi wa Mtaa wa Ihumwa, Zena Selemani alitoa faida za kutumia nishati safi ya kupikia jinsi zinavyoweka mazingira mazuri kwa mtoto ili asidhurike na moto na namna ambavyo inawapa fursa katika kufanya shughuli nyingine za maendeleo. “Gesi inanisaidia kupika chakula chochote kwa wakati hasa chakula cha mtoto, maana muda mwingine mtoto anaweza akawa anasumbua lakini ukienda kupika kwenye gasi unapika chakula chake kwa wakati na anakula kwa wakati. Kutumia nishati safi ya kupikia inanipa muda wa kutosha wa kuandaa chakula cha mtoto na cha familia. Kutumia nishati ya kupikia ya gesi au umeme, kiukweli chakula cha mtoto kinakuwa katika mazingira salama kwasababu hakuna zile athari za kurukiwa na moto maana muda mwingine mkaa unatoa moshi. Kwahiyo, ukitumia gesi, hizo athari zinakuwa hazipo” alisema Selemani.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.