WANAWAKE katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili waweze kukopeshwa fedha kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sharifa Nabalang’anya alipokuwa akihamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa katika uzinduzi wa kampeni ya uhamasishaji mkubwa wananchi iliyofanyika katika mtaa wa Mahomanyika uliopo kata ya Nzuguni jijini hapa.
Nabalang’anya alisema kuwa mfuko wa afya ya jamii ni muhimu zaidi kwa kina mama. “Kina mama tuwashawishi waume zetu sababu mara nyingi ndiyo washika fedha ili tujiunge na CHF na kuweza kupata huduma ya matibabu bure kwa watu 6 mwaka mzima kwa shilingi 30,000 tu” alisema Nabalang’anya. Mara zote ugonjwa haupigi hodi, hivyo wananchi wanatakiwa kujiandaa kukabiliana na ugonjwa kwa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa, aliongeza.
Kutokana na ukweli kuwa wanawake ndiyo wanaobeba jukumu kubwa katika familia, afisa maendeleo ya jamii huyo aliwashauri kujiunga katika vikundi. Alisema kuwa kujiunga katika vikundi kutawawezesha kupata mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo. Kupitia shughuli hizo za maendeleo kina mama wataweza kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa kwa kuchangia shilingi 30,000 na watu sita kuhudumiwa matibabu mwaka mzima, aliongeza.
Nae Katibu Tawala Wilaya ya Dodoma mjini, Edward Mpogolo alisema kuwa Rais wakati akinadi ilani ya uchaguzi aliahidi kuhakikisha wananchi wanajiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ili wawe na afya bora. “Kujiunga na CHF ni kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Magufuli za kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na afya bora” alisema Mpogolo.
Awali mratibu wa CHF katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Patrick Sebyiga alisema kuwa lengo la maboresho ya CHF ni kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanajiunga na mfuko huo ambao utawasaidia kupata huduma za afya kwa gharama nafuu.
Akiongelea hali ya wanachama, alisema kuwa idadi ya kaya zilizojiunga na mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa kuanzia Julai, 2018 hadi Juni, 2019 kwa kiwango cha shilingi 30,000 ni kaya 3,155. Idadi hiyo aliitaja kuwa ni sawa na asilimia 3.4 ya kaya zote zilizopo katika Halmashauri ya jiji la Dodoma.
Wananchi wa Mahomanyika wakimsikiliza Afisa Maendeleo ya Jamii wa Jiji Sharifa Nabalang'anya (hayupo pichani) wakati wa kampeni
ya kuhamasisha watu kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamaii ulioboreshwa.
Wakazi wa Mahomanyika wakimsikiliza Afisa Maendeleo ya Jamii wa Jiji (hayupo pichani) akifafanua faida za kujiunga katika vikundi
ili kupata mikopo na umuhimu wa kujiunga na CHF iliyoboreshwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.