VIKUNDI vya maendeleo ya wanawake katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma vimetakiwa kuwa mabalozi katika jamii juu ya umuhimu wa shughuli za kujiletea maendeleo ili wengine waweze kujiunga.
Ushauri huo ulitolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe alipoongoza Kamati ya Fedha na Uongozi kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo leo walipotembelea kikundi cha kina mama cha Juhudi.
Prof. Mwamfupe alisema kuwa wanufaika wa vikundi vya maendeleo wanatakiwa kuwa mabalozi kwa wengine kuhusiana na mafanikio ya kiuchumi yanayopatikana kupitia shughuli za maendeleo za vikundi. “Wapo wakina mama ambao wametulia na hawafanyi shughuli za uzalishaji mali. Ninyi mnatakiwa kuwa mabalozi kwa kuwaonesha na kuwaelezea umuhimu wa kujiunga katika vikundi na kufanya shughuli za uzalishaji mali” alisema Prof. Mwamfupe.
Aidha, alikitaka kikundi hicho kuzingatia usafi ili kutengeneza maandazi yaliyo katika ubora unaokubalika. “Pamoja na usafi katika shughuli zenu za kutengeneza maandazi ili kulinda afya za walaji, hakikisheni mazingira mnayofanyia kazi yanakuwa safi na mandhari yakuvutia” aliongeza Prof. Mwamfupe.
Awali mwenyekiti wa kikundi hicho, Zuhura Juma alisema kuwa kikundi hicho cha kutengeneza maandazi kinauwezo wa kutengeneza maandazi 7,500 kwa siku. “Mheshimiwa Mstahiki Meya, kikundi hiki kinatengeneza faida ya shilingi 50,000 kwa siku” alisema Juma.
Akiongelea mafanikio ya kikundi hicho, Juma aliyataja kuwa ni kufanikiwa kununua mashine ya kukanda unga wa ngano kwa ajili ya kutengeneza maandazi. Mengine ni kutoa ajira sita, kununua jiko kubwa la gesi kwa ajili ya kurahisisha shughuli za uchomaji maandazi na kuhifadhi mazingira.
Kikundi cha Juhudi kina wanachama watano na wafanyakazi sita, kilipatiwa mkopo wa shilingi milioni 10 na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia mfuko wa maendeleo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Utengenezaji wa maandazi katika kikundi cha Juhudi
Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe (kulia) akifurahia kazi za kikundi cha wanawake cha maendeleo kiitwacho Juhudi walipotembelea kikundi hicho na Kamati ya Fedha na Uongozi. Katikati (mwenye miwani myeusi) ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Sharifa Nabalang'anya.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.