WANAWAKE jijini Dodoma wametakiwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika michezo mbalimbali ili kuimarisha miili na afya zao.
Kauli hiyo ilitolewa na kaimu Mkurugenzi, Idara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Mboni Mgaza alipoongoza mamia ya wakazi wa Jiji la Dodoma kushiriki katika tamasha la michezo likiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea kilele cha siku ya wanawake duniani.
Mgaza alisema kuwa michezo ni muhimu katika kuimarisha afya na inasaidia kuimarisha mwili na kuusaidia kuepukana na maradhi nyemelezi. “Ukiwa mwanamichezo maradhi hayatakuvamia kwa sababu mwili utakuwa imara. Hivyo, michezo inaimarisha mwili na kuifanya akili kuwa timamu na kufikiria haraka tofauti na asiyeshiriki michezo” alisema Mgaza. Michezo inajenga mahusiano mazuri katika jamii kwa mtu mmoja mmoja na baina ya taasisi na taasisi, aliongeza.
Kwa upande wa mratibu wa tamasha hilo, Elizabeth Kasimila alisema kuwa aliandaa tamasha la michezo katika maadhimisho kuelekea kilele cha siku ya wanawake duniani ili kuwapa wanawake nafasi ya kushiirki michezo na kuweka miili yao katika hali nzuri.
“Leo, tumefanya mazoezi ya kutosha ili siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani tuwe na afya bora kushiriki maadhimisho ya siku ya wanawake duniani na kutembelea maeneo mbalimbali” alisema Kasimila.
Kasimila ambae pia ni Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Catalyst for Community Transformation Organization (CFCTO) alisema kuwa taasisi yake kwa kushirikiana na taasisi nyingine binafsi na serikali waliona jambo la mazoezi ni jema katika kujenga miili na afya ili kuepukana na maambukizi mbalimbali. “Kumekuwa na milipuko na maradhi tofauti, mtu akipata mafua kidogo anatetereka, hivyo tunaamini mazoezi ni tiba kwa mwanadamu” alisema mratibu huyo. Aidha, aliishukuru benki ya CRDB kwa kufadhili tamasha hilo.
Kwa upande wa mshiriki kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Elinajoyce Petro alisema kuwa michezo hiyo ni muhimu kwa afya. “Mazoezi haya ni muhimu kwa afya zetu kwa sababu yanatusaidia kujenga miili yetu, kujenga kinga ya mwili na magonjwa yasiyo ya kuambuliza yanazuiwa kwa kufanya mazoezi. Kwa wale ambao siyo watumishi wa umma wanakaribishwa kufanya mazoezi kila siku hapa uwanja wa Jamhuri kuanzia saaa 12 alfajiri” alisema Petro.
Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Wanawake katika uongozi, ni chachu kufikia dunia yenye usawa” na katika Jiji la Dodoma yatafanyika katika uwanja wa Nyerere Square.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.