Wanawake na wasichana waaswa kutoa taarifa za unyanyasaji wa kijinsia kwa wakati pindi wanapofanyiwa ukatili huo.
Hayo yalisemwa na Afisa Maendeleo ya Jamii Dawati la Kisheria, Rehema Mwalyambi wakati alipotembelea Kituo cha Redio A FM, wakati wa ziara ya wanawake wa Jiji la Dodoma katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni shamrashamra kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani, ambapo kwa mwaka huu maadhimisho yake kitaifa yatafanyika mkoani Arusha.
Mwalyambi alisema “wanawake wote pamoja na watoto wa kike tunaomba msiogope kutoa taarifa katika dawati la kijinsia lilipo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwasababu tunaona wanawake wengi wanaogopa sana kutoa taarifa pale wanapofanyiwa unyanyasaji wa kijinsia. Naomba sana msiogope kwasababu sasa hivi kuna haki kwa kila mtu awe mwanamke au mwanaume, kuna sheria na adhabu pia pale tuu mtu atakapofanyiwa vitendo ukatili. Sisi kama dawati la msaada wa kisheria tupo kwaajili ya kutoa msaada kwa wanawake wote wanaofanyiwa vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia”.
Nae, Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joyce Shija aliwatoa hofu wanawake na watoto kuhusiana na ukatili wa kijinsia, na kuwaahidi kuwa, endapo utatendeka ukatili wa kijinsia watapatiwa wanasheria kwaajili ya kufuatilia na kusimamia kesi zao.
“Niwatoe hofu wanaoogopa kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuhofia gharama. Dawati la maendeleo ya jamii linatoa huduma bure kwa kila mmoja na kila mtanzania ana haki ya kupata haki sawa. Hivyo basi, sisi tumejipanga vema kwaajili ya kukomesha unyanyasaji, kwahiyo wanawake wote tusiwe nyuma kupata haki zetu inabidi tupambanie kwasababu hivi sasa ni usawa kwa kila mmoja awe mwanaume au mwanamke tunahaki sawa” alisema Shija.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.