KAMATI ya Maandalizi ya siku ya wanawake Duniani Mkoa wa Dodoma imepanda miti 200 katika kituo cha Afya Mkonze na shule ya msingi Mkonze kwa lengo la kuihamasisha jamii kupanda miti kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kauli hiyo ilitolewa na mratibu wa kamati ya maandalizi ya siku ya wanawake duniani Mkoa wa Dodoma, Fatuma Daud alipokuwa akiongezea zoezi la upandaji miti lililofanywa na kamati hiyo kuelekea kilele cha siku ya wanawake duniani jana katika kata ya Mkonze.
Fatuma alisema kuwa kamati iliamua kwenda kupanda miti 100 katika eneo la shule ya msingi Mkonze na miti mingine 100 katika kituo cha Afya Mkonze. “Lengo la kupanda miti katika maeneo hayo ni kuihamasisha jamii kuona jukumu la kupanda miti ni la jamii nzima. Tumepanda miti 100 katika shule ya msingi Mkonze kwa lengo la kuifanya shule hiyo kuwa eneo salama kwa watoto kusoma, lakini pia kuwajengea wanafunzi wa shule hilo kuona wana wajibu wa kupanda na kutunza miti katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi” alisema Fatuma. Katika kituo cha Afya Mkonze, tuliona ni vizuri kuwa sehemu ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira ili kituo cha Afya hicho kiwe na mandhari na hali nzuri ya hewa ambayo kwa upande mwingine ni tiba kwa wagonjwa, aliongeza Fatuma.
Fatuma, ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema kuwa kamati ilichagua kwenda kupanda miti katika eneo hilo ukiwa ni mkakati wa kuwafanya wananchi wanaozunguka eneo hilo kuwa tayari kupokea tukio la kilele cha siku ya wanawake duniani. “Kilele cha siku ya wanawake duniani ngazi ya Mkoa wa Dodoma kitafanyika katika shule ya msingi Mkonze, hivyo zoezi la upandaji miti katika shule na kituo cha Afya ni kuwaandaa wananchi kupokea tukio hilo muhimu litakalofanyika Jumapili tarehe 8 Machi, mwaka huu katika shule ya msingi Mkonze” alisema mratibu huyo.
Kwa upande wake mkazi wa kata ya Mkonze Sikuzani Chogo alisema kuwa amefurahishwa na ushiriki wa watumishi wa serikali katika kupanda miti katika shule na kituo cha Afya. “Hata sisi wananchi sasa tunaona umuhimu wa kupanda miti kwenye maeneo yetu” alisema Sikuzani.
Zoezi la upandaji miti katika shule ya msingi Mkonze na kituo cha Afya Mkonze liliratibiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na wadau wengine. Maadhimisho mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kizazi cha usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya sasa na ya baadaye”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.