Na WMJJWM, Dar es Salaam
Wanawake nchini Tanzania wanaendelea kuwa nguzo imara katika kukuza na kuinua uchumi wa nchi katika sekta mbalimbali; ampapo asilimia thamanini (80%) ya nguvu kazi ya sekta ya kilimo ni wanawake na huzalisha asilimia sitini (60%) ya chakula nchini.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Khamis katika maadhimisho ya siku ya Mama na Mwana Disemba 2, 2023, Jijini Dar es Salaam.
Alisema katika baadhi ya familia, mwanamke ndio mhimili mkuu katika upatikanaji wa chakula, mavazi, malazi, huduma za afya, elimu na maji.
Aidha, Khamis amefafanua kwamba pamoja na majukumu yanayotekelezwa na wanawake katika familia na jamii zetu, bado zipo changamoto zinazowakwamisha ikiwemo vitendo vya ukatili .
“Vitendo vya ukatili vinasababishwa na uwepo wa mila na desturi kandamizi na zenye madhara, uwepo wa mfumo dume, ukosefu wa elimu, ushirikishwaji dhaifu katika ngazi za maamuzi, ukosefu wa elimu ya stadi za maisha pamoja na ukosefu wa mitaji ya utekelezaji wa shughuli za ujasiriamali.” Alisema Mwanaidi.
“Serikali imeendelea kutambua umuhimu wa Wanawake kupewa fursa katika nafasi za Uongozi na kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za uwakilishi na ufanyaji maamuzi, tunaye Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa kwanza mwanamke katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini pia yupo Dkt. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Ulimwenguni na takwimu zinaonesha kuwa idadi ya Mawaziri wanawake imeongezeka kutoka asilimia 15 mwaka 2005 hadi asilimia 36 mwaka 2022. Vilevile Wabunge wanawake wameongezeka kutoka asilimia 22 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 37 mwaka 2022.” Alisema Khamisi
Serikali inaendelea kupambana na changamoto ya ukatili katika jamii hususani ukatili dhidi ya wanawake na watoto kupitia afua mbalimbali za kijamii ikiwemo kutungwa kwa sheria za fedha, uanzishwaji wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi na kuendeleza mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.