Wanawake nchini wametakiwa kuondokana na dhana ya kuwa tegemezi na wajiingize katika ujasiriamali ili kujikwamua kiuchumi, tukielekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yenye kauli mbiu isemavyo “Kizazi cha usawa kwa maendeleo ya Tanzania ya sasa na ya baadaye”.
Hayo yamesemwa na baadhi ya wanawake Jijini Dodoma, ambapo Husna Juma, binti mjasiriamali alieleza jinsi alivyothubutu na kuanzisha biashara ya kuuza uji na chai na kwamba ndiyo inayomwezesha kuendesha maisha yake.
Husna ambaye ni mama wa watoto wawili anaendesha maisha yake kwa biashara hiyo huku akiwasomesha kutokana na kipato anachokipata katika biashara hiyo.
Alizungumza namna alivyoiona fursa na kuichangamkia alisema “Mimi ni kijana tena mthubutu ambaye niliiona fursa na kuamua kuichangamkia, nilikuwa nauza vocha lakini kuna mama mjamzito alinishawishi, tulikuwa tukifanya kazi jirani kila nikifika ananiuliza kama nimemletea uji” alisema.
Aliendelea kwa kusema kuwa, “Siku ya kwanza nakumbuka nilikuja na chupa moja tu kwa ajili yake lakini cha kushangaza yeye aliambulia kikombe kimoja tu, hapo nikaona fursa nikapata moyo wa kuingia katika biashara hii ambayo wadada wengi hawawezi kutokana na kuidharau”, alisema Juma.
Mbali na fursa hiyo aliyoiona na kuifanyia kazi, pia amekiri uwepo wa changamoto ambazo anakumbana nazo katika biashara yake hiyo hali ambayo mara nyingine inamkatisha tamaa ya kuendelea na kazi hiyo.
“Kazi hii ni ngumu kutokana na mazingira ninayofanyia kazi, wengi wananidharau kwa kile ninachokifanya na kuniona kama napoteza muda, lakini kujiamini kwangu na bidii ndiyo iliyonifikisha hapa.
“Nakumbuka biashara hii nilianza mwaka 2013 nikiwa na mtaji wa 15,000 lakini hivi sasa nimefikisha mtaji wa laki mbili, hivyo niwashauri tu wanawake wenzangu tusichague kazi, ilimradi tu ni halali na inakupatia kipato, ili tuondokane na utegemezi”, alisema mjasiriamali huyo.
Aidha alitoa wito kwa wanawake kuelekea machi 8 mwaka huu ambayo ni siku ya wanawake duniani kuhakikisha wanashiriki ipasavyo katika shughuli zitakazowainua kimaendeleo ili kuweza kuitetea 50-50 ya usawa baina yao na wanaume katika nyanja zote.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.