Na. Dennis Gondwe, KIKOMBO
WANAWAKE wametakiwa kuacha ukatili wa kimwili kwa watoto badala yake wawalee katika maadili mema na kumjua Mungu.
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa Viti Maalum Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Edith Luhamo alipoongea na wananchi na wanafunzi wa Kata ya Kikombo jijini Dodoma.
Luhamo alisema “kina mama tumekuwa ni walezi wa familia zetu, kina mama tumekuwa tukikaa na watoto wa waume zetu, tumekuwa tukikaa na watoto wa kaka zetu au watoto wengine ambao wazazi wao wametangalia mbele za haki lakini tunawafanyia ukatili. Watoto wamekuwa wakipigwa fimbo kupitiliza watoto wamekuwa wakichomwa moto. Kina mama tuwe na roho ya huruma ambayo tumeumbiwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Tatizo kina mama tumegeuka kuwa wakatili namba moja na hasa ambao siyo watoto wetu. Tuachane na huo ukatili tunazalisha kizazi ambacho hakitatufaa huko mbele. Tutakuwa tunatengeneza bomu na siyo kizazi kizuri” alisema Luhamo.
Alisema kuwa wanawake wamekuwa sehemu kubwa ya ukatili unaodhuru mwili kwa watoto kutokana na vipigo na kuwachoma moto watoto. “Unakuta mtoto ana njaa kaenda kuchukua wali uliolala jana mnamchoma moto. Hii haikubaliki. Sasa hivi kuna wimbi la ushoga na usagaji, ni janga kubwa kwa taifa. Tunategemea tumezaa watoto ili nao watuletee uzao baadae tukiachia vitendo hivi kuendelea tunaharibu kizazi kijacho wenyewe. Kwa wakristo unapoenda kanisani jitahidi kuwahimiza watoto wako kwenda kanisani kule watajifunza neno la Mungu na kuwa watoto wema. Kwa waislam, unapoenda msikitini himiza watoto waende, kule watajifunza neno la Mungu” aliongea kwa uchungu Luhamo.
Aidha, aliwataka wakina mama kujikita katika malezi ya watoto. “Ukiona mtoto ana nyendo tofauti tofauti kina mama tusaidiane malezi. Ukiona mtoto wangu ana nyendo tofauti niambie au palepale muadhibu na unipe taarifa. Kila mtu ana ndoto yake, wanangu wanafunzi wa kike tusikubali kudanganyika na vichipsi na lifti za bodaboda” alisema Luhamo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.