Na. Faraja Mbise, DODOMA
Wanawake watakiwa kujitathmini katika nyanja za uongozi kwa kuonesha nia ya kuwajibika ipasavyo na kuchangamkia fursa za uongozi zinazojitokeza katika jamii.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alipokuwa akizungumza na maelfu ya wanawake waliojitokeza katika kongamano la kanda ya kati lililohusisha mikoa mitatu (Dodoma, Singida na Iringa) katika kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani kongamano hilo lilifanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, Dodoma.
Senyamule alisema “naomba nitoe shime kila mmoja wetu ajitathmini hatua gani amechukua kuonesha uwezo wake wa kuongoza katika eneo alilopewa. Ni imani yangu kuwa kila mahali tunatosha kwasababu Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha uwezo wa kutosha kwenye nafasi ya urais. Kwahiyo, wanawake tunaweza katika kila eneo”.
Akiongelea kuhusu takwimu za wanawake viongozi wa Mkoa wa Dodoma, alisema karibu ngazi zote za uongozi kuna viongozi wa kike na takwimu zinaonesha uthubutu ni mdogo na hivyo aliwataka wanawake kuongeza uthubutu wa kuwanania nafasi hizo za uongozi.
“Mkuu wa mkoa kwa sababu anatakiwa mmoja, kwahiyo ni asilimia 100 inaongozwa na mwanamke, kwa wakuu wa wilaya ni asilimia 71, kati ya wakuu wa wilaya saba wawili ni wanaume na watano ni wanawake na wanafanya vizuri katika nafasi zao. Tukienda upande wa wabunge, asilimia 11 ni wanawake, katibu tawala tuna asilimia 86, wakurugenzi wa halmashauri asilimia 25 na madiwani asilimia 14 za wanaogombea ni wanawake” alisema Senyamule.
Kwa upande wake, Mfamasia kutoka Hospitali ya Rufaa, Mkoa wa Dodoma, Jackline Moshi, alisema kuwa amejifunza mengi katika kongamano hilo na kuchangamkia fursa zinazojitokeza katika jamii.
“Tumejifunza mengi sisi kama wanawake, tukayafanyie kazi hasa kujiamini katika nyanja mbalimbali za uongozi, kujiamini katika kufanya kazi, kujiamini katika kila sekta. Tukisimama na wanaume tunaweza” alisema Moshi.
Nae, mkazi wa Dodoma, Rhobi Maro alisema amevutiwa sana na rai iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule na Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anna Makinda ya kuchangamkia fursa katika uongozi. Pia alitoa rai yake kwa wanawake kuendelea kujiamini na kupambana kuchangamkia fursa zinazojitokeza.
“Wameongelea kuchangamkia fursa kujitokeza hasa katika kugombea na kupambana zaidi. Na tunaamini wanawake wengi watajitokeza katika uchaguzi huu wa 2025 kugombea nafasi mabalimbali za uongozi. Natoa rai kwa wanawake wote waendelee kupambana na kujiamini kwamba wanaweza” alisema Maro.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.