WANUFAIKA wa mpango wa kunusuru kaya masikini katika Kata ya Uhuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameshauriwa kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF) iliyoboreshwa kwa shilingi 30,000 ili watu sita waweze kupata huduma ya matibabu bila malipo kwa mwaka mzima.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Nala, Monica Lugaila alipokuwa akiongea na wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini katika Mtaa wa Kipande, uliopo Kata ya Uhuru jijini hapa.
Lugaila alisema kuwa mfuko wa afya ya jamii (CHF) iliyoboreshwa ni muhumu kuwahakikishia uhakika wa matibabu kwa kipindi cha mwaka mzima. Alisema kuwa mtu au watu wanaweza kujiunga na kukata CHF iliyoboreshwa na kupata huduma ya matibabu kwa watu sita kwa mwaka mzima kwa gharama ya shilingi 30,000 tu. Suala la afya ni muhimu kwa kila mtu, maandalizi ya mapema kabla ya kuugua ni muhimu ili kuepuka kutumia gharama kubwa pindi anapougua, aliongeza.
Aidha, Afisa huyo alisema kuwa zoezi hilo la uhawilishaji fedha linafanyika kwa wanufaika waliohakikiwa katika kipindi cha uhakiki tarehe 30 Julai, 2020 ndiyo wanaohusika na zoezi hilo. “Katika zoezi hili, hakuna utaratibu wa kuchukuliana fedha, kila mnufaita alitakiwa kuchukua fedha yake mwenyewe. Kwa wale wanufaika ambao hawakuweza kufika kutokana na sababu mbalimbali kama ugonjwa, tuliwafuata nyumbani na kila mmoja alilipwa malipo anayostahili na kusaini kwa mujibu wa taratibu” alisisitiza Lugaila.
Akiongelea utekelezaji wa zoezi la uhawilishaji fedha, mratibu wa tasaf Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sekunda Kasese alisema kuwa zoezi hilo limepangwa vizuri. “Kwa siku ya leo, zoezi la uhawilishaji fedha litafanyika katika mitaa 28, iliyopo katika kata 13 za Jiji la Dodoma. Katika mitaa hiyo, jumla ya wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini 1,645 wanatarajia kupokea malipo ya shilingi 104,828,000. Nikumbushe tu kuwa zoezi hili litahusha madirisha mawili ya malipo yaani awamu mbili zitalipwa kwa pamoja” alisema Kasese.
Kwa upande wake mlengwa wa mpango wa TASAF, Tatu Ndala, alisema kuwa zoezi hilo la uhawilishaji fedha lilifanyikavizuri na kwa uwazi. “Watu wa TASAF walipofika kwanza walitupa mafunzo na kutuhamasisha kuhusu CHF iliyoboreshwa na watu wasiokuwa na namba za NIDA waliorodheshwa majina yao ili kuwasaidia kupata namba hizo. NAona safari hii walikuwa wamejipanga vizuri sababu hapakuwa na msongamano wa wat una mambo yalienda haraka haraka. Mimi namshukuru sana Mungu kwa sababu TASAF imenisadia sana kuanzisha shughuli ya Mama lishe ambayo inaniwezesha kuishi kwa uhakika” alisema Ndala.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.