WASHEREHESHAJI nchini wametakiwa kuzingatia miiko na maadili ya tasnia hiyo katika kutekeleza majukumu yao ili kuendelea kuaminika katika jamii.
Kauli hiyo ilitolewa na mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dodoma, George Rujabuka alipokuwa alielezea umuhimu wa washereheshaji kuzingatia maadili ya tasnia hiyo katika maonesho ya Nanenane, Nzuguni jijini hapa.
Rujabuka alisema kuwa tasnia ya ushereheshaji ni muhimu katika jamii kwa sababu ndiyo inabeba dhana nzima ya sherehe.
“Mimi ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu chuo kikuu cha Dodoma lakini pia ni mshereheshaji ninayefahamu na kufuata maadili na miiko ya kazi ya ushereheshaji. Maadili ya ushereheshaji ni lazima ujue kwamba shughuli yoyote lazima ichukuliwe kwa uzito mkubwa. Mfano, tupo katika maonesho ya Nanenane, mahudhui lazima yaendane na shughuli ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na mambo mengine” alisema Rujabuka.
Katika utekelezaji wa jukumu hilo, alisema suala la matumizi ya lugha yenye staha kwa makundi yote, muonekano wa mavazi na itifaki ni mambo ya msingi sana katika ushereheshaji, alisisitiza. “Tasnia ya ushereheshaji inaenda sambamba na muziki, tunatumia muziki kuwaburudisha watu. Katika banda letu, nipo na Eric Mchomvu yeye ni ‘DJ’ mbobezi. Tunatumia muziki kuwaburudisha watu na sisi ni wataalam tunajua tucheze muziki gani kulingana na huduma zinazotolewa kwa kufuata itikadi na taratibu za eneo husika. Muziki tunaotumia ni ule unaowavuta watu usio na viashiria vya kukashifu dini, kabila, au mtu” aliongeza Rujabuka.
Akiongelea huduma zinazotolewa na chuo kikuu cha Dodoma, alisema kuwa zinatolewa huduma za afya bure katika eneo la upimaji, ushauri na elimu ya afya. Upimaji unaofanyika ni wa shinikizo la damu, virusi vya ukimwi, uwiano wa uzito na urefu na magonjwa ya ini na figo.
Huduma nyingine aliitaja kuwa ni udahili katika ngazi ya shahada ya uzamili na uzamivu zinazofanyika katika banda hilo.
Aidha, aliwakaribisha wananchi wa Jiji la Dodoma kutembelea banda hilo na kunufaika kwa kupata huduma za afya bure.
Maonesho ya nanenane Maonesho ya nanenane mwaka 2020 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kwa maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi, chagua kiongozi bora 2020”.
mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dodoma, George Rujabuka alipokuwa alielezea umuhimu wa washereheshaji kuzingatia maadili ya tasnia hiyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.