WASHIRIKI wa maadhimisho ya siku ya makazi duniani wametakiwa kutumia fursa ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuwa makao makuu ya nchi na kununua viwanja mapema ili kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Magufuli.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge alipomuwakilisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Taifa ya Takwimu jijini hapa.
Dkt. Mahenge alisema kuwa Jiji la Dodoma ndiyo makao makuu ya nchi. Katika kuboresha makazi ya wananchi, michoro 748 imekwishaandaliwa yenye viwanja zaidi ya 300,000 vya matumizi mbalimbali, alisema. “Nitoe wito kwenu washiriki wa maadhimisho haya ya siku ya makazi duniani na wanachi wote kwa ujumla kuchangamkia fursa ya viwanja katika Jiji la Dodoma. Viwanja vipo vya kutosha ambavyo vimepimwa tayari, fika ofisi ya Jiji hata leo ili uwe sehemu ya mafanikio ya uwekezaji huu mkubwa unaofanywa na Rais, Dkt. John Magufuli” alisema Dkt. Mahenge.
Mkuu wa Mkoa alisema kuwa serikali imeandaa sera ya nyumba iliyobainisha changamoto na namna ya kuwezesha jamii kuwa na nyumba bora. “Sera hii inatoa dira ya uendelezaji wa sekta ya nyumba nchini, juhudi zitaelekezwa zaidi kwenye mbinu mbalimbali za kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kupata nyumba zilizo bora. Aidha, serikali imeweka mazingira wezeshi kwa taasisi zisizo za kiserikali katika uboreshaji wa nyumba za makazi. Baadhi ya taasisi hizo zimekuwa zikishiriki katika uboreshaji wa nyumba za makazi yasiyokuwa rasmi” alisema Dkt. Mahenge.
Kwa upande wake, Afisa Mipango miji wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Aisha Masanja alipokuwa akiwasilisha mada juu ya uboreshaji wa makazi ndani ya Jiji la Dodoma katika maadhimisho hayo alisema kuwa Halmashauri imetekeleza kwa asilimia 80 uboreshaji wa makazi yaliyokuwa holela ndani ya Jiji la Dodoma pamoja na kupanga makazi mapya. “Tunahakikisha kila kipande cha ardhi ndani ya Jiji la Dodoma kinapangwa na kupimwa ili kulinda Jiji kwa sasa na miaka ijayo kwa mipango endelevu ya matumizi ya ardhi, kuhifadhi ardhi na kuboresha makazi kwa kila mkazi wa Dodoma na nchi kwa ujumla” alisema Masanja.
Ikumbukwe kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa mahitaji ya nyumba yanaongezeka kila mwaka kwa takribani nyumba 200,000.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.