Na. Faraja Mbise, DODOMA
WASIMAMIZI wa miradi ya ujenzi katika Shule ya Sekondari Matumbulu wametakiwa kuwa wazalendo na kutokwamisha juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alipokuwa akikagua miradi ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Matumbulu iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Matamanio ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuleta hizi shule ni kwasababu watoto wasitembee umbali mrefu. Bado sisi Mkoa wa Dodoma tuna utoro na baadhi ya changamoto inayochangia utoro ni watoto kutembea mwendo mrefu kwenda shule. Kwahiyo, anaona fahari asiende shuleni. Lakini tuna ukatili wa kijinsia, kati ya maeneo ambayo watoto wanafanyiwa ukatili ni akiwa anaenda shuleni, wanapita maporini kwasababu ya umbali mrefu, yote haya Rais ametaka ayamalize kwa kuwajengea shule karibu na eneo lao” alisema Senyamule.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Wilaya ya Dodoma, Sakina Mbugi, alitoa rai kwa wafanyakazi kuweka mbele uzalendo ili kuhakikisha miradi hiyo inasonga mbele kwa wakati na kwa viwango vya juu. “Ni rai kwa wenzangu na mimi mwenyewe, tuweke mbele uzalendo ili tuweze kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati, kwa viwango vilivyokusudiwa na kuzingatia thamani ya fedha ili tuweze kufikia lengo lililokuwa limekusudiwa” alitoa rai Mbugi.
Mradi huo wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Matumbulu unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 31, Mwaka huu. Shule hiyo ilitengewa jumla ya Shilingi Milioni Mia tano arobaini na nne, laki mbili, ishirini na tano elfu na mia tano ishirini na sita (544,225,526) kwa ujenzi wa miundombinu ya shule ikiwa ni pamoja na madarasa nane na ofisi mbili yanayogharimu shilingi 192,628,542, Jengo la Utawala shilingi 71,491,667, Maabara ya Fizikia 50,000,000 Maabara ya Baiolojia na Kemia 100,000,000, Jengo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) 56,969,143, Choo shilingi 18,700,000, Kichomea taka 3,833,333 na Tanki la maji 3,641,667.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.