Na. Dennis Gondwe, MTUMBA
WASIMAMIZI wa vituo vya kupigia kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na uzalendo wakizingatia kanuni na taratibu ili kuweza kufanikisha uchaguzi huo.
Kauli hiyo ilitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Dkt. Frederick Sagamiko alipokuwa akifungua mafunzo kwa wasimamizi wa vituo vya kupigia kura, tukio lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali Mtumba.
Dkt. Sagamiko alisema kuwa wasimamizi hao wapo kwa ajili ya kuapishwa na kupewa mafunzo kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kutokana na sifa na uwezo wao katika utendaji kazi ndiyo zimewafanya waweze kuchaguliwa. “Tunahitaji kuongeza umakini na usikivu wakati huu wa mafunzo. Hata kama ulisimamia uchaguzi uliopita, huu ni wa mwaka 2024 na haujawahi kufanyika popote. Hivyo, kuna utofauti kati ya uchaguzi huu na uchaguzi uliopita. Moja ya mabadiliko ni mabadiliko ya kanuni, niwasihi muongeze umakini katika kusikiliza ili tusiende kuharibu uchaguzi huo. Miongoni mwa mambo ambayo hutakiwi kucheza nayo ni uchaguzi. Uchaguzi unatoa hatima ya usalama na utulivu wa taifa letu. Maendeleo yanategemea hali ya usalama katika Jiji letu. Hivyo, tekelezeni jukumu hili kwa kuzingatia uzalendo” alisema Dkt. Sagamiko.
Wakati akiwakaribisha alisema “karibuni kwenye ukumbi maridhawa na bora kabisa wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma hapa Mji wa Serikali Mtumba. Niwapongeze kwa kupata nafasi kuteuliwa kuwa wasimamizi wa vituo kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Jiji lina watumishi zaidi ya 5,000 na mliobahatika ni kama 1,050. Ni kutokana na weledi wenu, sifa zenu na uzalendo wenu kwa taifa letu. Leo mtaapishwa, mkaishi kiapo ili kiwe dira na makatazo ya mambo ambayo hamtakiwi kufanya wakati wa uchaguzi” alisema Dkt. Sagamiko.
Nae Mwakilishi wa Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) Mkoa wa Dodoma, Zacharia Mwandumbya aliwataka wasimamizi wa vituo vya kupigia kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 kutojihusisha na vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo. “Ni vema mtakapoapishwa mkafanye kazi kwa uadilifu kama mlivyoelekezwa na viongozi wenu” alisema Mwandumbya.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.