Na. Faraja Mbise, DODOMA
Wasimamizi wa vituo vya kupigia kura katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameaswa kuviishi viapo vyao walivyoapa ili wawe na muongozo mzuri pindi watakapokuwa katika vituo vyao vya kazi ifikapo tarehe 27 Novemba, 2024.
Hayo yalisemwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipokuwa akifungua semina ya wasimamizi wa vituo vya kupigia kura iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali Mtumba.
“Mtaenda kuapishwa, naomba mkaishi kiapo mtakachokipata, ili iwe dira na ndio yawe makatazo ya mambo ya kutokufanya wakati wa usimamizi” alisisitiza Dkt. Sagamiko.
Akiongelea kuhusu kanuni na taratibu za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, aliwasisitiza wasimamizi wa vituo vya kupigia kura, kufuata kanuni za uchaguzi za mwaka huu 2024, kwasababu ni tofauti na kanuni za uchaguzi uliopita. Hivyo, aliwataka kuwa makini ili wasifanye makosa ifikapo tarehe 27 Novemba, 2024. “Najua wapo waliowahi kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019, Naomba niwaambie tunahitaji kuongeza umakini na usikivu wakati huu wa mafunzo, hata kama ulikuwa umesimamia mwaka 2019, uchaguzi huu ni wa mwaka 2024 na haujawahi kufanyika popote, utafanyika tarehe 27 Novemba, 2024. Na kama ni wafuatiliaji yapo mengi ya tofauti kati ya chaguzi za Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu. Moja ya tofauti ni mabadiliko ya kanuni. Kanuni zilizotumika katika uchaguzi wa 2019 na chaguzi nyingine kabla ya hapo ni tofauti sana na kanuni zinazotumika mwaka huu. Hivyo, niwasihi muongeze umakini katika kusikiliza ili tusiende kuharibu siku hiyo. Bahati nzuri wengi wenu ni walimu na miongoni mwenu mlishawahi kusimamia kazi maalumu na sisi tunasema miongoni mwa mambo ambayo hautakiwi kucheza nayo mojawapo ni uchaguzi, nafikiri ni miongoni mwa yale mambo makuu ambapo ukipata nafasi ya kushiriki unakosa usingizi ni pamoja na uchaguzi. Uchaguzi unatoa hatima ya usalama na utulivu wa taifa letu. Maendeleo ya sehemu yoyote yanategemea sana hali ya usalama katika eneo husika” alisema Dkt. Sagamiko.
Akiongelea kuhusu sifa na vigezo vilivyotumika kuchagua wasimamizi wa vituo vya kupigia kura, alikanusha madai ya kuwa wasimamizi hao walichaguliwa kwa upendeleo. “Leo mtapata mafunzo mafupi lakini pia zoezi kubwa la kuapishwa, kuwa rasmi kwenda kusimamia vituo vyetu kwa siku ya uchaguzi. Ninajua wapo wenzenu ambao waliwauliza kwanini mimi nimekosa na wewe umepataje? wengi wanaweza wakahisi kwamba kuna watu juu yenu waliofanya muwe hapo lakini niwahakikishie ni sifa zenu ndizo zilizowafanya muwe hapo” alisisitiza Dkt. Sagamiko.
Aidha, aliwapongeza wasimamizi wa vituo vya kupigia kura kwa kuchaguliwa kuwa miongoni mwa wasimamizi wa vituo siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. “Niwapongeze sana kwa kupata nafasi ya kuteuliwa kuwa miongoni mwa wasimamizi wa vituo siku ya tarehe 27 Novemba, 2024 kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Jiji la Dodoma lina watumishi takribani 5,000 tano ‘plus’ na mliobahatika takribani 1,450 na, mnaweza mkaona ni namna gani mchujo ulikuwa mgumu, lakini niwaambie tu ni kutokana na weledi wenu, sifa zenu na uzalendo wenu kwa taifa letu, ndio maana leo mpo hapa kwa ajili ya kupata mafunzo mafupi lakini kwa tukio kubwa kabisa la kuapishwa” alipongeza Dkt. Sagamiko.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.