WATAALAM wa Maabara na Watarajali nchini wametakiwa kuzingatia maadili na taaluma zao ili kutoa huduma iliyobora kwa wananchi.
Msajili wa Baraza la Wataalamu wa Maabara Nchini Mary Mtui ameyasema hayo leo alipotembelea wataalamu na watarajali wa maabara katika hospitali za KCMC na Mawenzi mkoani Kilimanjaro
“Mnatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Miiko na maadili ya taaluma ikiwa ni kipaumbele kwa wataalamu wa maabara ili kutoa mchango wa huduma bora katika sekta ya afya utakaopelekea kuwa na msaada chanya kwa wagonjwa,” alisema Mtui
Aidha, Mtui amewakumbusha watarajali wakati wote wakiwa kwenye mafunzo kuhakikisha wanakuwa na log book zao zikiwa zimejazwa sehemu ambazo ameshapita kufanya mafunzo ya utarajali ili zipatikane pale zitakapohitajika kwa ajili ya ukaguzi.
Mtui amesisitiza ushirikiano na mahusiano mazuri baina ya wasimamizi na watarajali wenyewe kubadilishana uzoefu wa kitaalamu pale inapohitajika kwa lengo la kuboresha mafunzo.
“Lakini pia sio vibaya tukashirikishana baina ya kituo kimoja na kingine ili tufikie lengo la kutoa majibu yenye ubora kwa kuboresha sekta ya afya na kuipaisha taaluma hii ya maabara,” alisema Mtui
Sambamba na hayo Mtui amewataka Wasimamizi kuimarisha usimamizi kwa watarajali, ikiwa ni pamoja na uongozi wa maabara kuhakikisha wanaimarisha mahusiano mazuri ya kazi kati ya wasimamizi na watarajali ili kuwa na mazingira rafiki ya mafunzo kwa pande zote.
Mwisho, amewasisitiza Watarajali kutumia vyema fursa waliyoipata kwa kuhakikisha wanapata ujuzi na umahiri ambao utaenda kuleta matokeo chanya ya huduma bora kwa wananchi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.