Na. Aisha Ibrahim, DODOMA
KAIMU Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo, aliwataka watumishi wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi, kuongeza wigo kwa kutumia wataalam wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Maendeleo ya Jamii ili kuhakikisha wanasambaza taarifa za uhamasishaji na kubainisha watoto wenye mahitaji maalumu katika jamii.
Fungo aliyasema hayo ofisini kwake alipopokea taarifa ya ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalumu kwa mwaka 2025 kutoka Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Jiji la Dodoma baada ya kukamilika zoezi la utambuzi na ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalum kwa jili ya kuandikishwa elimu ya awali na darasa la kwanza zoezi lililoanza 07 hadi 22 Januari, 2025.
Akitoa pongezi kwa kazi nzuri ya ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalumu, Kaimu Mkurugenzi, alisema kuwa serikali inafanya juhudi kubwa kuhakikisha watoto hao wanapata haki stahiki na huduma za msingi ili kujiona wako sawa na binadamu wengine. “Mpaka serikali inafanya juhudi kubwa ya namna hii, maana yake kuna eneo ambalo watu wamejisahau na kuwaweka watoto hawa pembeni, lakini ni watu ambao wanastahiri huduma kama zile ambazo sisi tunapata” alisema Fungo.
Aidha, aliongeza kuwa Halmashaurii ya Jiji la Dodoma, imejipanga kwa kutekeleza mradi mkubwa wa Kituo cha Mafunzo ya Sayansi ili kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kujifunza kwa vitendo mambo mbalimbali kulingana na ewelewa wake binafsi. “Dodoma sasahivi tunafikiria mambo makubwa na tuna mradi mmoja ambao tunatarajia kutekeleza Kituo cha Mafunzo ya Sayansi. Kwahiyo, watoto watakao kuwa wanaingia pale watakuwa wanaangaliwa, huyu ana uwelewa gani? Kama ni kompyuta basi apelekwe sehemu husika na kama ana uwelewa wa magari basi apelekwe huko” alisema Fungo.
Kwa upande wake Afisa Elimu, Elimu Maalumu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Issa Kambi alichanganua kuwa katika ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalumu, idadi yao jumla ni 218. Alisema watoto saba walipewa rufaa ya kwenda hospitalini kutokana na changamoto maalumu za kiafya. Watoto 37 walipaswa kujiunga na shule maalumu, na kati ya hao, watoto 11 walitakiwa kwenda shule jumuishi, na 39 walipangiwa kwenda vitengo maalumu lakini pia watoto 11 walipangwa kwenda vyuo vya ufundi Singida kutokana na umri wao wa kujiunga na elimu ya shule ya msingi kupita.
Sambamba na hayo, alisema katika zoezi hilo walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kupata watoto wengi katika kata mbalimbali ikiwa ni kutekeleza agizo la Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma la uandikishaji na ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalumu shuleni kwa ngazi ya awali na msingi. “Tumefanikiwa kupata watoto wengi wenye mahitaji maalumu na wenye kuhitaji hafua stahiki kama ambavyo tumeziwasilisha kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma” alisema Mwl. Kambi.
Licha ya kuwepo mafanikio, Mwl. Kambi alisema kuwa katika zoezi hilo wamekutana na changamoto mbalimbali ikiwemo uhamasishaji duni ndani ya kata husika, idadi iliyozidi kwa watoto kuanzia miaka 14, baadhi ya watendaji wa kata kutoa maelezo yasiyo jitosheleza, uwelewa mdogo wa jamii kuhusiana na haki za watoto wenye uhitaji maalumu, mtazamo hasi kwa watoto hao kuhusu suala la elimu na uwezo duni wa wazazi kuwapatia matibabu stahiki watoto hao.
Pia, aliwashauri wazazi na walezi ambao bado hawajapeleka watoto wao katika zoezi la ubainishaji, kuwapeleka watoto hao katika shule zilizopo karibu yao ili wahusika wa zoezi hilo waweze kupata taarifa kamili. “Ushauri wangu kwa wazazi ambao bado hawajawaleta watoto kuwabainisha na pengine hawakupata taarifa vizuri wakati tunapita kwenye kata hizo, wawapeleke kwenye shule zilizopo maeneo jirani ili kusudi wale walimu waweze kutupatia taarifa mfumo wa ubainishaji ili tuweze kufika na kuwabaini hao watoto” alisema Mwl. Kambi.
Lakini, aliiomba serikali kukamilisha na kuboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na kuongeza bweni lingine la Hombolo, litakalo watengenezea mazingira rafiki watoto hao kupata elimu bora ili kuendana na mahitaji yao. “Tunaomba tuweze kupata bajeti ya kuweza kujenga bweni lingine jipya, kwasababu watoto hawa wanaongezeka kila kukicha” aliomba Mwl. Kambi.
Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kufuatilia zoezi la uandikishaji na ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalumu kuwa endelevu ili kuhakikisha watoto wanapata huduma zote za msingi na haki stahiki kama binadamu wengine.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.