Wataalamu wa Mifugo wametakiwa kutumia taaluma zao na kushiriki kikamilifu katika kubuni mbinu za kisasa za kuinua viwango vya minyororo ya thamani ya mazao ya Mifugo na Uvuvi ili kuleta tija na kukidhi mahitaji ya uchumi wa viwanda kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Amos Zephania alisema hayo alipokuwa akifungua Kongamano la 43 la Kisayansi la Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi na Mkutano wa 44 wa mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo Tanzania linalofanyika jijini Dodoma kuanzia Desemba 2- 4, 2020.
Zephania alisema kuwa Serikali imedhamiria kuanzisha na kuendeleza viwanda mbalimbali hususani vya uzalishaji na usindikaji wa mazao ya kilimo na mifugo ambavyo ni msingi wa maendeleo endelevu.
“Serikali inatambua kuwa maendeleo ya viwanda hapa nchini yatachagiza upatikanaji wa bidhaa muhimu na bora kwa matumizi ya ndani na nje ya nchi jambo ambalo litainua ubora na viwango vya maisha ya wananchi, kujenga uchumi imara na kukuza uchumi wa Taifa unaoweza kuhimili ushindani wa kikanda na kimataifa,” alisema Zephania.
Aliendelea kusema kuwa ni wazi kwamba mifumo ya uzalishaji wa mifugo na uvuvi katika nchi yetu imeegemea zaidi katika uzalishaji kwa mifumo ya asili ambapo wazalishaji wengi ni wafugaji na wavuvi wadogo wadogo.
Aliongeza kuwa mifugo mingi iliyopo bado ni ya asili ambayo tija katika uzalishaji wake hairidhishi huku akisema kuwa ngómbe wengi wa asili wana uzito mdogo wa kati ya kilo 200 hadi 350 ambao hupelekea kutoa maziwa kidogo na nyama kidogo ambayo haizidi wastani wa kilo 175.
Kufuatia hali hiyo, Zephania alisema kuwa Wataalamu wa Mifugo wanajukumu la kufanya kuleta mabadiliko katika mifumo ili kuongeza ufanisi na tija ya uzalishaji kwa kutumia sayansi na teknolojia za kisasa huku akiwasisitiza kuwasaidia wafugaji waweze kuongeza ubora wa uzalishaji ili mali ghafi za uhakika ziweze kupatikana kwa matumizi ya viwanda vya kusindika mazao ya mifugo na uvuvi.
“Huu ni wakati mwafaka wa kufanya mapinduzi makubwa katika minyororo ya thamani ya mifugo na samaki ili kukidhi mahitaji ya uchumi wa viwanda tunaouzungumzia kwa sababu mahitaji ya lishe ya protini inayotokana na mifugo yanatarajiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka 20 ijayo kutokana na ongezeko la idadi ya watu, kukua kwa miji na kuongezeka kwa kipato cha watu,” aliongeza Zephania
“Hivyo ni lazima uzalishaji wa mifugo na samaki uboreshwe ili kukidhi mahitaji haya, wahimizeni wafugaji na wazalishaji kuwekeza katika teknolojia na vitendea kazi sahihi vitakavyowaongezea uzalishaji mashambani mwao na kuwawezesha kufikia masoko kwa ufanisi zaidi,”alifafanua Zephania
Aidha, Zephania aliwahimiza wataalamu hao kuendelea kuimarisha afya za mifugo, usimamizi wa mifumo bora ya uzalishaji na kutoa huduma za ugani kwa wakati sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya masoko ikiwemo uhifadhi, usafirishaji na usambazaji wa mazao hayo huku akisema kuwa mazao ya mifugo na uvuvi yanaharibika upesi yasipotunzwa na kuhifadhiwa ipasavyo.
Naye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Maduka Kessy alisema kuwa jukumu la Wataalamu hao ni kuinua tija na faida kwa wafugaji wanaoshiriki katika uwekezaji kwenye mnyororo mzima wa thamani.
Kessy aliongeza kuwa Mkoa wa Dodoma una zaidi ya Kaya Mia nne na Hamsini Elfu (450,000) na kati ya kaya hizo Asilimia 44 ni wafugaji na ndio wenye kipato cha chini na maendeleo yao ni duni, hivyo kuna haja ya kuwaendeleza ili waweze kunufaika na mifugo yao.
“Dodoma ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kuwa na mifugo mingi, mpaka sasa takwimu zinaonesha tuna ng’ombe milioni 1.8 lakini mnyororo wa thamani kwa mifugo hiyo ni mfupi sana, hivyo kuwepo kwenu hapa leo ni faraja ya kwamba mtakuwa chachu ya mabadiliko kwa wafugaji wetu ili waweze kufaidika na mifugo yao,” alisema Kessy
Kessy aliendelea kusema kuwa mfumo wa ufugaji kwa wananchi wengi umepitwa na wakati huku akiongeza kuwa kasi ya ukuaji wa mji wa Dodoma ni kubwa hivyo kuna haja ya kutafuta namna ya kuchangamanisha ukuaji wa mji na maendeleo ya sekta ya mifugo.
Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Amos Zephania akiongea na washiriki (hawapo pichani) wakati akifungua Kongamano la 43 la Kisayansi la Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi na Mkutano wa 44 wa mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo Tanzania (TSAP) unaofanyika jijini Dodoma kuanzia Desemba 2- 4, 2020.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Maduka Kessy akitoa salamu za Mkuu wa Mkoa wa Dodoma katika Kongamano la 43 la Kisayansi la Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi na Mkutano wa 44 wa mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo Tanzania (TSAP) unaofanyika jijini Dodoma kuanzia Desemba 2- 4, 2020.
Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Amos Zephania (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Washiriki wa Kongamano la 43 la Kisayansi la Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi na Mkutano wa 44 wa mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo Tanzania (TSAP) unaofanyika jijini Dodoma kuanzia Desemba 2 - 4, 2020. Kutoka kulia ni Makamu Mwenyekiti wa TSAP, Dkt. Imna Malele, wapili kutoka kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Maduka Kessy na watatu ni Mwenyekiti wa TSAP, Dkt. Daniel Komwihangilo. Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Dkt. Jonas Kizima, wapili ni Kaimu Mkurugenzi, Uzalishaji na Masoko, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Stephen Michael na watatu ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Uwekezaji (TIB), Dkt. Maria Mashingo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Mifugo Tanzania (TSAP), Dkt. Daniel Komwihangilo (kushoto) akimkaribisha mmoja wa washiriki wa Kongamano la 43 la Kisayansi la Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi na Mkutano wa 44 wa mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo Tanzania (TSAP) unaofanyika jijini Dodoma kuanzia Desemba 2- 4, 2020.
Mmoja wa Wadau wa Kongamano la 43 la Kisayansi la Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi na Mkutano wa 44 wa mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo Tanzania (TSAP) akipokelewa na kusajiliwa kwa ajili ya kushiriki Kongamano hilo linalofanyika jijini Dodoma kuanzia Desemba 2- 4, 2020.
Sehemu ya Washiriki wa Kongamano la 43 la Kisayansi la Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi na Mkutano wa 44 wa mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo Tanzania wakifuatilia matukio yanayojiri katika mkutano huo unaofanyika jijini Dodoma kuanzia Desemba 2- 4, 2020.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.